Siku ya jana nimeshinda nikilia baada ya kusoma makala yako kuhusu namna ya kudhibiti hasira zako. Nimelia nikimkumbuka Kaka yangu, kila siku tulikua tukisema ana hasira za karibu na hakufanya chochote kuzidhibiti.
Nakumbuka ilikua ni siku ya Jumamosi, Kaka alikuja nyumbani kumsalimia Mama na baada ya hapo akatuambia twende wake ili tukawachukue watoto alitaka kututoa out. Tuliondoka, mimi, Kaka na mdogo wangu mwingine wa kike mpaka kwa Kaka Tabata.
Tayari Kaka alishampigia mkewe simu ili awaambie watoto wajiandae kwani anawapitia, nakumbuka walibishana kidogo kuhusu chakula, wifi aksiema ameshapika Kaka kwa hasira akamuambia utakula mwenyewe mimi natoka na ndugu zangu.
Nakumbuka nilimuambia kwanini tusitoke na wifi na jibu lake lilikua “Ule mzigo tuupeleke wapi? Atatuhatibia siku yetu tu!” Alimaliza na tulipofika nyumbani watoto hawajaandaliwa alinza kumfokea mkewe na kidogo ampige lakini nilimuangalia kwa jicho la kumsuta akaacha.
Aliongea ongea tu maneno ya kumfokea, mkewe alikua ameweka kitu jikoni hivyo alienda na mtoto mkubwa wa kike kipindi hicho ana mika kumi alienda kumuandaa mdogo wake wa miaka minne, huku mtoto mwingine wa Kaka wa miaka saba yeye akiwa chumbani.
Tukiwa tumekaa na Kaka sebuleni tunasubiri watoto watoke, tulisikiakelele kutoka jikoni. Ilikua ni sauti ya wifi. “Mamaa nakufa!” Alipiga kelele, wote tulinyanyuka kasoro Kaka na baada ya zile kelele tulisikia kishindo Puuuu! Mimi na mdogo wangu tulikimbia mpaka jikoni.
Inaelekea aliungua wakati anaepua kitu, kwani kitambaa kilidondoke kwenye jiko na kuanza kuunga. Tulikiondoa, lakini inaelekea wakati anajiondoa kwenye moto alikanyaga mchi mdogo wa kutwangia akateleza na kupiga kichwa chini.
Damu zilikua zinamtoka puani na mdomoni, nilimuita Kaka ambye hakujali sana akaja, kumuona vile alistuka, akainama pale chini kujaribu kumnyanyua lakini alionekana kupoteza fahamu ingawa mapigo ya mbali yalisikika kwa mbali.
“Kawashe Gari!” aliniambia huku akiinama na kumchukua mkewe, nilichukua fungu ambazo nilikua nazo kwenye pochi na kwenda kuwasha gari. Wakati huo Kaka alimbeba mkewe, wakati anapita sebuleni mtoto wake mkubwa alimuona alivyombeba Mama yake.
Alimvamia na kuanza kulia, umempiga Mama, Mama! Mamama! Alimuita Mama yake bila kuitikia, alitoka nnje na kuanza kupiga Kelele, “Baba kamuona Mama, Baba kamuua Mamaa!” Alipiga kelele kwa hasira huku akilia kwa nguvu. Wapangaji ambao walikua mabanda ya uani walitoka kuangalia.
Walimuona kweli Kaka akitoka kambeba shemeji damu zinachuruzika, ghafla walinza kupiga kelele na kutaka kumvamia Kaka. Alijaribu kuwaelewesha lakini hawakusikia, Kaka alikimbia harakaharaka na kuingia kwenye Gari, niliwsha Gari na kuanza kwenda Hospitalini.
Yulifika, walitaka PF# lakini hata hivyo baada ya kumuangalia wifi slishafariki muda mrefu kwnai alidondoka na kuangukia kisogo, ubongo uliingia damu. Ilibidi twende Polisi ambao walikuja, tuliwaelezea kilichotokea lakini walipofika nyumbani waliambia stori tofauti.
Kaka alikamatwa na kuweka ndani, mtoto wake alikua analia na kusisitiza kuwa Baba yake kamuua Mama yakie kwani kila siku alikua anakimpiga na siku ile alimtukana kwa kuchelewa kuwaandaa ili kutoka wote.
Majirani nao walipohojiwa walisema ni akwaida sana ya Kaka kumpiga mke wake na walishaongea sana, alishampiga na kumvunja mkono, akampiga na kumuumiza jicho. Mwili wa wifi ulipochunguzwa ulikutwa na makovu tena mabichi mgongoni, alikokua anachapwa na mikanda na Kaka yangu.
Nikweli hata sisi tulikua tunajua kuwa Kaka anampiga mkewe, mara nyingi wifi alishalalamika lakini tulimuambia vumilia. Alisharudi kwao zaidi ya mara tatu lakini mara zote Kaka huenda kuomba msamaha na kusema hatarudia ila alirudia tena.
Kwa hali ilivyokua ingawa sisi tulikua upande wake na tulijua kilichotokea lakini hakuna mtu ambaye alitamini. Wote walijua tunamtete kwakua ni Kaka yetu. Watoto walikua wanalia tu na kumlaumu Baba yao kuwa ndiyo kamuua Mama yao, hakuna aliyetaka kuuelewa ukweli.
Kaka alsihitakiwa kwa mauaji, tulijaribu kila kitu ili kesi isiende mahakamani lakini wapi? Ndugu za wifi walikomaa, na kesi iliendeshwa kama miaka minne akakutwa nahatia, alihukumiwa kunyongwa, tulikata rufaa lakini wapi.
Ni mwaka wa kumi sasa, Kaka yangu yuko jela kwakosa ambalo hakulifanya. Anasubiri tu sahihi ya Raisi ili kunyongwa kwani tushamaliza rufaa zote. Watoto wake hawataki hata kumuona Baba yao, wanaamini ni muuaji na kwakua sisi tunamtetea basi wamehamia upande wa Mama yao na hawataki kujua chochote kuhusu sisi.
Naomba ufiche jina langu, najua itawaudhi baadhi ya ndugu zangu lakini nimeona niandike kwani hizi hasira zitakufikisha pabaya. Kaka asingekua mtu wa kumpiga mkewe watu wangemuamini, lakini kutokana na tabia zake mpaka watoto wake wanajua leo kuwa ni muuaji na anasubiri kunyongwa.
Kila nikiwaza kilichotokea huwa nalia tu, nakosa amani yaani hata kumchapa mtoto naogopa kwani kila saa picha ya wifi inanijia. Nikweli alimtesa sana wifi yangu lakini hakumuua. Natamani hao watu wanaojifanya wana hasira wangesoma makala yako na kujua namna ya kuzidhibiti kwani majuto ni mjukuu.
****MWISHO
0 Maoni