HESHIMU HESHIMA ILIYOBEBWA NA MWENZAKO, HESHIMU BARAKA ILIYOBEBWA NA MKEO.

Image result for sexiest

Muhali gani wapenzi wa uwanja huu wa saikolojia na mahusiano ni muda mrefu sijasema nanyi kwasababu ya pilika za hapa na pale, Mungu awabariki wote mnaoendelea kufuatilia makala hizi ili kuboresha mahusiano yetu.
Leo nimeona nizungumzie hili la heshima kwa mume na baraka kwa mkeo kwasababu siku hizi maisha watu wamegeuza fasheni, ndoa nyingi zinaishi kwa maigizo, watu wengi wanaishi maisha mabaya kwasababu wametengeneza laana ndani ya nyumba badala ya baraka.
Mpenzi msomaji, Mungu alipoitengeneza ndoa ya kwanza alitoa jukumu kwa kila upande ili kutengeneza kanuni inayofikika na kwamba wanandoa hao waishi kwa hizo kanuni.
Unapoolewa unakuwa umebeba kusudi la mumeo kufanikiwa au kutofanikiwa kwasababu baraka na laana zinatoka kwa mke mwenyewe. Kwanini!!?
Ndoa/mahusiano yanapokuwa katika hali ya utulivu, kusikilizana, utii, upendo, furaha, amani hapo Mungu hutazama sana namna ya kushusha baraka kwasababu mnakuwa katika mstari unaokusudiwa.
Lakini pia shetani naye huwa macho kutaka kuharibu kwasababu ibilisi hapendi kuona mwanadamu aliye upande wa Mungu anabaki kwenye upande huo ndio maana leo hii watu wanaweza kuanza mahusiano vizuri lakini baada ya muda mfupi, kukaanza mkanganyiko eidha kwasababu ya maneno ya uchochezi kutoka nje au kiburi na majivuno kutoka kwa mmoja wa wanandoa.
Usipokuwa makini unaweza kumlaumu sana mwenza wako kuwa yeye ana tatizo wakati na wewe pia una tatizo hilohilo, ndugu zangu unapoamua kuingia kwenye ndoa hakikisha masikio yako unaweka pamba tena mpya zisizopitisha hata upepo.
Kwasababu kwa dunia hii ya sasa tusitarajie kupata watu wakamilifu lakini wenzi bora wapo kila kona ni namna gani tu unatengeneza mahusiano yako katika upekee na sio kugeuza mahusiano kuwa fasheni na maonyesho kwenye mitandao ya kijamii, hili linawafanya wengi waishi kwa namna mitandao inavyotaka na sio katika ubora wa mahusiano ulivyo.
Walichobaki nacho ni kubadilisha status tu kila siku baada ya kuachwa na kubebwa na mwingine kisha kuachwa tena. Maisha ni vile ulivyoyatengeneza wewe na mwenza wako, usilazimishe kuishi kistaa wakati uwezo wako ni wa dona tembele.
Mwanaume anapooa anakuwa amemheshimisha mwanamke na ndio maana mahali popote mwanamke aliyeolewa akijitambulisha jina pekee huwa haimpi heshima kuliko akisema yeye ni mke wa fulani au Mrs. fulani.
Vivyo hivyo kwa mwanaume anapokuwa na mke kila milango ya baraka hufunguliwa kwasababu ya yule mke aliye naye, ni rahisi sana kukuta mwanaume aliyekuwa masikini baada ya kuoa kuanza kupata mali ni kwa sababu ya baraka za mkewe hivyo kila mmoja atambue wajibu wake kwenye mahusiano.
Mwanaume mpende mkeo, mwanamke mtii mumeo wala usiache kumstahi kwa lolote, kutangulia kufanikiwa kwa mwanamke hakuondoi nafasi ya mwanaume kwenye maisha yako hata kama mumeo atakuwa masikini asiye na kitu, usijenge kiburi kwa vichache ulivyonavyo kuna vingi Mungu ameweka kwa ajili yenu simama kwenye nafasi yako.

Chapisha Maoni

0 Maoni