Kama wewe ni mwanamke na ulishawahi kuniomba ushauri kuhusiana na matatizo yako ya kimahusiano nitakuwa nimekuuliza shili swali hili “Unafanya kazi?” Kama sikukuuliza basi jua uliniambia unafanya kazi au nilipitiwa tu. Niswali muhimu sana kwangu kwani naamini kuwa kama uko huru kikipato basi kukubali kunyanyaswa na mwanaume ni mapenzi yako.
Kwamba kuna wanawake wengi wapo kwenye ndoa za mateso na hawawezi kutoka si kwakua hawataki lakini kwakua hawana pakwenda kwani wanawategemea wanaume kwa kila kitu. Kwa bahati mbaya zaidi hii ni silaha kubwa ambayo wanaume wengi huitumia kuwanyanyasa wanawake, kwamba kama mwanaume anajua kuwa mkewe haendi popote kwakua hana kipato basi humnyanyasa zaidi.
Hii haimaanishi kufanya kazi hapana, kuna wanawake wengi ambao hufanya kazi lakini hawako huru kikipato na hili ndiyo tatizo kubwa. Kwamba unafanya kazi na una mshahara mzuri au unabiashara yako lakini haupo huru kikipato. Hapa nikimaanisha kuwa, una matumizi ambayo wewe mwenyewe huwezi kuyamudu kutokana na kipato chako.
Lakini mbaya zaidi nikuwa wakati mwingine unaona shida kuishi kutokana na kipato chako. Kwa mfano unafanya kazi ambayo haitosho hata kumsomesha mwanao mmoja katika shule anayosoma sasa, huwezi kujaza mafuta gari ambayo unaendesha achilia mbali kulinunua. Hapa unafanya kazi lakini kiuhalisia nikuwa nilazima umnyenyekee huyo mwanaume ili kuishi maisha unayoishi sasa.
Mwanaume akishakujua kua uko hivyo basi nirahisi kukunyanyasa, hii ndiyo maana wakati mwingine unawaza hivi yule dada si ana kazi yake kwanini haondoki anateseka vile. Ukweli unakuja kuwa kazi yake haiwezi kumlisha au kumhudumia kwani ana matumizi makubwa kuliko kipato chake.
Lakini kuna wale ambao hawafanyi kazi kabisa za kipato, hawa ndiyo hawawezi kuchoka kabisa, hawa wanalazimika kuvumilia kwani ukweli nikuwa kama wakiondoka sio tu wanashindwa kujiendesha maisha yao hata kama wangetaka kupunguza matumizi, lakini ukweli nikuwa wanaenda kuwa mizigo kwa ndugu.
Hawa ndiyo wale unakuta kaachika anarudi kwao kuwa mzigo, kaachika anaenda kwa Kaka yake ambaye kaoa kwenda kumharibia ndoa yake na kuwa mzigo. Hawa mara nyingi hulazimika kuvumilia mateso kwani wanajua kuwa wakiondoka kwa mume basi wanafuata mateso mengine ya ndugu ambayo yanaweza kuwa machungu zaidi.
Kama uko katika hali hii nilazima ili kuishi bila kunyanyasika basi jifunze namna ya kuwa huru kikipato.
0 Maoni