
Najua unajidanganya kuwa anakupenda, si anakuhudumia tena kuliko mkewe na anakuambia kabisa kuwa alikosea kuoa angekutana na wewe mapema basi angekua na furaha, anakuambia namna ambavyo ndoa yake haina amani na anakuambia kuwa akiwa na wewe anajisikia vizuri, anakupa kila kitu unachotaka na unaona fahari, unajiona mke na hata anamdharau mkewe mbele yako.
Ndiyo Dada yangu unafuraha na unaina maisha ndiyo hayo, anakuhudumia kuliko hata kale kaboyfriend kako, anakuambia anapenda watoto. Labda kakuambia umzalie, lakini labda hajakuambia ila unaona ili kumkomoa mkewe lakini labda ili upendwe zaidi na kumshikilia kabisa na hata ili uolewe unambebea mimba sasa kabla hujafanya huu upuuzi kumbuka mambo haya.
(1) Hata Mkewe Alikua Anampenda Kama Wewe; Usidhani kama alimuoa mkewe akiwa naamchukia alikua anampenda na kumuonyesha mapenzi kabla ya kumuoa na kumzalisha na sasa kamtelekeza. Najua unajihisi spesho lakini ukweli nikua wewe si spesho mko wengi kama yeye na hata mkewe alikua hivyo hivyo. Sasa ukishamzalia na wewe utakua kama mkewe tu kuwa si mchepuko tena binti bali Mama watoto wake!
Najua unajihisi uko spesho na nina uhakika kwa mambo aliyokuambia ushajisemea “Mkewe ana matatizo!” Ila niamini mimi nishasikia hizi stori nyingi, huna uspesho wowote tena inawezekana wewe una matatizo kuliko mkewe, hivyo usidhani kama ukishazaa na kuanza kuomba matumizi atakuvumilia, hapana atakimbia majukumu na utakuja kulea mwenyewe hivyo hembu jiandae kwa hilo!
(2) Nirahisi Kulea Mchepuko Kuliko Mchepuko Na Mtoto; Sasa hivi mambo anayofanya kwako anaamua, ni starehe na mnafurahia wote ndiyo maana anafanya. Lakini ukilogwa ukabeba mimba tu unaacha kuwa starehe unageuka na kuwa majukumu kama mkewe, kwamba hafanyi tena kwakua anataka bali kwakua ni lazima na unakua kero kuomba matumizi kama mkewe!
Labda nikupe mfano sasa hivi kama mchepuko anaamua kukununulia gauni, anaamua kukutoe out na kukupa hela ya saluni. Hivyo kama siku hana basi anaweza kukuambia hana na ukamuelewa. Lakini akishakuja mtoto basi jua kuwa mtoto hawezi kuacha kula, hawezi kuacha kuumwa eti kwakua Baba hana pesa, nakuambia kuwa ukizaa naye utakua majukumu sawa na mkewe watu hukimbia majukumu na si starehe atakukimbia!
(3) Huyo Ni Mtu Wa Kukwepa Majukumu Na Kuwasingizia Wengine; Kama alimtelekeza mkewe akaja kwako jua kuwa huyo ni mkwepa majukumu hivyo ukishamzalia atakukimbia na kwenda kwingine ambapo hakuna kelele za mtoto, hakuna majukumu ya lazima. Mambo yakiwa magumu atakukimbia na kwenda kwingine ambako ni kwepesi kama alivyomkimbia mkewe na kuja kwako, utaanza kuwa kero kama mkewe.
Kwamba alikua anakusimulia mkewe ana kelele, kumbuka kelele za mkewe nikwakua alikua anamuambia anunue chakula, awahi nyumbni kuona watoto wasimsahau Baba yao, asalimie ndugu zake, atoe matumizi. Sasa hivi wewe humuambii hivyo vitu kwakua ni mchepuko, ukishazaa naye anaacha kuwa mchepuko na kuwa Baba wa wanao hivyo utaanza kumuambia hivyo vitu na atakukimbia kwani utakua kama mkewe.
(4) Wanajitambua Na Kurudi Kwa Wake Zao; Siku akijitambua na kurudi kwa mkewe sharti la kwanza litakua ni kuacha kuwasiliana na wewe, Kama ni mstaraabu sana atamchukua mwanae na kwenda kulea na mkewe akisha samehewa na wewe itakua basi. Lakini kana ni sheteni basi atakuachia mtoto, atajifanya kutunza ila atakavyo banwa na mkewe atakutelekeza kimyakimyakama wewe unavyosoma hapa kimya kimya kwa aibu.
Nataka nikuambie kitu kimoja, anakuambia anakupenda kweli, pengine kuliko hata mke wake, lakini kama hawezi kumuacha mke wake kwaajili yako. Kama atasingizia watoto, ndoa ya kanisani na kusingizia chochote kile kuwa hawezi kumuacha mkewe kwaajili yako basi jua hakupendi vyakutosha. Kwa maana hiyo nikuwa siku akili zikimrudia atarudi kumuomba msamaka mkewe na wewe utakua yule shetani uliyempitia angekua anakupenda angemuacha mkewe!
Tena wakati mwingine hamuachi mkewe kwakua michepuko mko wengi hivyo hawezi kuwachagua wote, anamtukana, na anampiga lakini mwanamke haondoki tena wengine mwanamke akitaka kuondoka wanatishia kuchukua watoto. Najua wewe mchepuko unasikia raha anavyomtukana mkewe mbele yako na hata kumpigia simu mkewe na kumtukana, lakini nikuambie kitu kama hajamuacha basi hajakupenda hata kama anakulamba miguu jiandae na kutelekezwa.
(5) Ukikubali Kuzaa Na Mume Wa Mtu Kubali Kulea Peke Yako; Haijalishi kakuambia nini unatakiwa uwe na akili kua huyu ni muongo kwani hata mkewe hakumuambia nitachepuka hivyo hembu acha kujibebesha mimba ukidhani utahudumiwa ukibeba ndiyo umebeba imekula kwako akikutelekeza hakuna namna ni kupambana na hali yako tu! Narudia kama wewe ni mchepuko basi wewe ni mchepuko ndiyo hadhi yako hata kama anakufanya ujihidi mke!
Kuwa mchepuko ni kama Pilipili, ni tamu sana ikiwa kwenye kachumbari tena kwa Chips au ikiwa kwenye Nyamachoma. Lakini kamwe si tamu kama ukiila kwenye chakula, mwanaume yeyote anayechepuka ukishazaa unaanza kuwa kama chakula wakati wewe ni Pilipili. Utaanza kudai haki za mke, mtoto kusomeshwa, kupigiwa simu, kuhudumiwa na vitu kama hivyo, utakera na atakutelekeza, kama anajidai anakupenda muambie muache mkeo ndiyo uje kunizalisha uone kama hatakimbia!
Najua Dada zangu mkishapenda mnachanganyikiwa zaidi, mnajiona special na kuhisi labda mnakitu cha ziada kuliko hao wake zao. Kwamba labda nyie sijui mmeumbwa na udongo wa mbinguni na mkewe kaumbwa na udongo wa chooni! Lakini nikuambie kitu kama huamini wewe beba mimba yake ikifikisha miezi sita basi atakukimbia utakuja kuniomba ushauri na mimi nitakuambia ununue Kitabu changu kwanza, hamna namna si unapendwa sasa Beba tu!
0 Maoni