Mwaka jana nilimfumania mume wangu na binti wa kazi, walikua wanafanya mapenzi sebuleni, nilienda kumshitaki kwa wazazi wake, alikataa katakata pamoja na binti wa kazi kusema kuwa kweli miimba ni ya mume wangu. Kwakua yule binti alikua na miaka 16 mume wangu alianza kunitangaza kuwa nimepanga na binti wa kazi ili kumfunga.
Alinisingizia kuwa nina lengo la kumtengenezea kesi ya ubakaji, alinichafua sana, tulirudi nyumbani akawa haongei na mimi. Alinipiga sana siku hiyo na kuniambia nirudi kwetu kwakua mimi ni mnyama hivyo naweza kumuua, cha ajabu hakutaka binti kuondoka na nilipoondoka yeye na Mama yake walimchukua yule binti na kwenda kumtoa ile mimba.
Nilijua kwakua ilimsumbua sana mpaka akalazwa hospitalini mwezi mzima, walianza kusema kuwa mimi ndiyo nimemloga na maneno mengi sana. Lakini nilivuimilia, nilikaa nyumbani miezi mitatu, mwanaume hakunitafuta, hakupiga simu wala kutoa matumizi kuhudumia mtoto. Alikua akijitapa kwa watu kuwa nitarudi kwa magoti na hawezi kuomba msamaha mchawi.
Baba yangu alimpigia simu kujua hatima yangu lakini alijibu majibu ya hovyo sana, niliumia sana kuona Baba yangu anatukanwa. Rafiki yangu mmoja alinielekeza kwako na kuniambia niongee na wewe. Nilikupigia simu kukuomba namna ya kunisaidia kurudiana na mume wangu kwani pamoja na yote nilikua bado nampenda, tulikua na mtoto, pale nyumbani maisha yalikua magumu na niliona kabisa wameanza kunichoka.
“Wakati mwingine mapenzi hayatoshi kuwa na mtu, wakati mwingine uvumilivu haumaanishi kudumu kwa ndoa, kila mtu utakayekutana naye atakuambia ndoa ni uvumilivu rudi kwa mume wako kapige magoti atakusamehe. Lakini mimi nakuambia ndoa ni furaha, hata ukirudi kwa mume wako leo kama huna furaha basi kesho atakuja kukuacha kwa sababu ya kijinga tu!
Lakini huwezi kuwa na furaha kama haupo huru kikipato. Mwanamke unapoondoka kwa mume na kurudi kwenu mwanaume anakua hajali kwakua anajua piga ua utarudi kwake, anajua kuwa ndugu watakuchoka kukuhudumia. Ushauri wangu, kama unataka mume wako kukurudia anza kuwa na furaha, anza kujitegemea, kwanza tafuta kazi.
Najua ajira ni ngumu lakini tafuta kazi yoyote, baada ya kuwa na kazi, ukishapata kitu kidogo basi tafuta chumba chako hama na mwanao, kuwa na maisha yako, kama mwanaume bado anakupenda atakutafuta kwakua ataogopa kukupoteza lakini kama hakupendi basi atakuacha kwakua hatajali tena kama ukimuacha, ukiwa bado upo kwenu mwanaume anajua kuwa huendi popote hivyo hata hajali chochote”
Mimi nina elimu ya digrii, lakini kupata kazi ilikua shida sana, kazi yangu ya kwanza ilikua ni kwa Mama lishe, pale iringa mjini stendi, na digrii yangu nilikua nalipwa shilingi elfu mbili kwa siku. Nilihangaika mjini, mume wangu anapita tena makusudi ananiona ananityumia meseji kunitukana kuwa nitaangaika sana lakini sikujali, nilifanya kwa moyo mmoja kwani kwangu ilikua bora kuliko kukaa nyumbani.
Nilifanya ile kazi ya Mama lishe kwa miezi mitano, nikajikusanya ndiyo nikapata mtaji kama wa laki mbili, baada ya ule mtaji niliamua kuhama, nikawa ninanunua madera na vijora, nilikua nachukua Dar naleta hapa Iringa, nilifanya kwa miezi miwili faida ikawa ndogo, mtaji ukakata nikawa sina hata shilingi kumi, nilirudi tena nyumbani, nikahangaika kwa ndugu ndugu nikapata elfu kumi.
Hiyo ilikua kama nauli, nikaenda mtera, kuna Mama mmoja alikua anauza samaki, anachukua mtera anazungusha vijijini, nilifika na elfu kumi kama nauli. Hapo mtoto nimemuacha kwa Mama. Pale nilikua sina mtaji tena, ilikua sifuri, lakini nilianza kumsaidia yule Mama kukaanga samaki, alikua ananipa elfu mbili kwa siku, nilifanya ile kazi kwa miezi minne. Mwaka huu mwezi wa sita ndiyo na mimi nilipata mtaji wa kununua samaki.
Nanunua samaki Mtera nazungusha vijijini, Kaka nakuhsukuru kwa kunivumilia na kutokuniruhusu kukata tamaa. Nadhani mimi ndiyo nilikua mteja msumbufu kuliko wote, kwa zaidi ya mwaka na nusu nimehangaika, lakini sasa hivi upepo umekua wangu. Nilijikusanya na mtaji wa laki mbili lakini nilikua nazungushia laki moja tu, ila nilianza kutengeneza wateja wangu tangu zamani.
Mama niliyekua na mkaangia na kumkaushia samaki alikua ananiacha nazunguka, kuna kipindi alikua ananipa kijiji flani nenda, nikawa na wateja wangu, sasa hivi faida naiona, kusema kwel, nina miezi mitatu tu lakini nimenunua kiwanja changu, sio cha bei ghali ni laki tano tu lakini ni changu na namshukuru Mungu.
Saa nimekuandikia kwakua mume wangu alijua kuwa nimenunua kiwanja, si akaanza kufuatilia na kujua kuwa nina Biashara nina pesa zangu. Sasa hivi anaanza kunisumbua kuwa eti anataka mtoto, ananiambia kuwa siwezi kumuacha mtoto kwa Mama nirudi niache biahsara yangu niamue kurudi kwake kulea mtoto au amchukue mtopto. Nilimuambia kabisa kuwa siwezi kuacha kazi na kwa mazingira niliyopo basi siwezi kwenda na mtoto.
Aliniambia atamchukua nikamjibu kuwa mtoto ni wake kama anataka aende akamchukue, alikasirika na kutishia kumchukua kweli. Juzi akaja nyumbani, akataka kuimchukua, nikagoma nikaenda ustawi wa jamii. Amefika kule anabwabwaja kuwa anamchukua kwakua mimi siwezi kumlea, anaulizwa yeye anawezaje akasema kuwa anampelekea Mama yake.
Anaulizwa kuna tofauti gani mtoto kulelewa na Mama yake au Mama yangu kabaki kimya anaishia kusema tu kuwa ni Mama yake anamuamini zaidi. mimi wakati wote huo namuangalia. Kumjua Kaka Iddi raha, kipindi anagoma kumhudumia mtoto uliniambia nimtumie meseji za kuomba matumizi kila baada ya siki moja, akiziona meseji nyingi lazima atajibu utumbo.
Akigoma niende ustawi wa jamii, katika kiindi cha mwaka nilienda ustawi wa jamii mara tatu na zote aliitwa na kugoma kuja. Alipomaliza kuongea nilitoa simu yangu, nikaonyesha meseji zake zote za matusi kuhusu mtoto, namna ambavyo hawezi kumhudumia, aliyokua anatukana na hata kusema kuwa labda mtoto si wake. Nilikumbusha tarehe ambazo nilienda ustawi wa jamii akaitwa na kugoma kuja.
Alibaki mdomo wazi akashindwa chakuongea, pale pale nilipewa mtoto mimi na kuambiwa kama akigoma kuhudumia basi niende mahakamani. Tuliondoka akiwa na hasira, juzi alinitafuta na kuniomba tuongee sisi wawili. Nilieda na kumsikiliza, baada ya kuongea sana aliniomba msamaha na kuniambia kuwa alifanya makosa, anataka kurudiana na mimi, aliomba msamaha sana nikamuaamini ndipo nimeamua kuja kwako Kaka kukuuliza kama kabadilika au la?
JIBU LANGU; Katika maisha huwezi kujua kama mtu kabadilika au la, kama mtu kajuitia au la? Huwezi kujua nafsi ya mtu, lakini unaweza kujua nafsi yako, msamehe mume wako si kwakua kabaidlika bali kwakua wewe umebadilika, kwamba zamani alikuambia usifanye kazi ukakubali, ulikua ni ujinga, rekebisha ujinga wako kwa kusema kuwa piga ua siachi kazi yangu.
Mwanzoni alikua anatembea na wanawake mbele yako unachekea, badilika kwa kusema kuwa siwezi kukubali, nikiona unaendelea kutembea nao mbele yangu siliii tena na amua kuwa na maisha yangu. mwanzoni alikua anakupiga, badilika kwa kusema kuwa ukinigusa naanzia polisi kisha kila mtu kivyake. Kama wewe kwenye nafsi yako unajiona umebadilika basi msamehe.
Humsamehi kwakua unaona kabadilika hapana, yeye anaweza kuigiza bali msamaha wako ni kwakua unajua kabisa kuwa wewe umebadilika na huyumbishwi yumbishwi tena. Usirudiane naye na kuanza kutafuta makosa, kwamba kwakua alishakusaliti bali kila dakika ni kuchunguza kana kwamba unamlazimisha kuchepuka a kukukosea, hapana hapo hutakua na amani, samehe, sahau lakini usiwe mjinga ili uwe na amani.
0 Maoni