FUNZO LA BIBI



Image may contain: 1 person, sitting
FUNZO LA BIBI
Binti mmoja mwanandoa alienda kwa bibi yake na kumweleza kuhusu maisha yake na jinsi mambo yalivyo magumu kwake – huku akimlalamikia kuwa mumewe alikuwa amemsaliti na hivyo alikuwa amekanganyikiwa. Hakujua la kufanya, akataka kukata tamaa na kuachana na ndoa. Alikuwa amechoka kupigana na kugombana mara kwa mara. Ilionekana kuwa pindi tatizo moja linapotatuliwa, basi tatizo lingine huzuka.
Bibi alimchukua na kumpeleka jikoni. Alichukua sufuria tatu, akajaza maji na kuziweka kwenye moto. Muda mfupi tu sufiria hizo zikachemka. Katika sufiria ya kwanza aliweka karoti, katika sufuria ya pili akaweka mayai, na katika sufuria ya mwisho akaweka mbegu za kahawa. Aliziacha zichemke huku akiwa kimya kabisa.
Baada ya takribani dakika ishirini aliipua sufuria. Alizitoa karoti na kuziweka kwenye sahani. Aliyatoa mayai na kuyaweka kwenye sahani. Akaitoa kahawa na kuiweka kwenye kikombe maalum.
Alimgeukia mjukuu wake na kumuuliza: “Unaona nini hapa?”
“Ninaona karoti, mayai na kahawa”, alijibu.
Bibi alimwambia asogee karibu zaidi na kuzigusa karoti. Alifanya kama alivyoambiwa na kubaini kuwa karoti zile zimekuwa laini. Bibi akamwambia achukue yai moja na kulimenya. Baada ya kutoa ganda la juu, alibaini kuwa kiini cha ndani kimekuwa kigumu.
Kisha bibi akamwambia aonje kahawa. Mjukuu alitabasamu baada ya kuonja kahawa na kuhisi harufu yake maridhawa. Akauliza: “Bibi, nini maana ya zoezi hili?”
Bibi akamfafanulia maana ya vitu hivyo ambavyo vyote viliwekwa kwenye mtihani wa aina moja: MAJI YA MOTO. Kila kimoja kilikuwa na mwitikio tofauti kabisa. Karoti ambayo mwanzo ilikuwa ngumu na madhubuti, baada ya kuwekwa kwenye maji ya moto ililainika na kuwa dhaifu. Yai ambalo ni tete na lenye kuvunjika upesi, gamba lake la nje lilikuwa limeyalinda majimaji yake ya ndani, lakini baada ya kuwekwa kwenye maji ya moto, kiini chake cha ndani kikawa kigumu. Hata hivyo, mbegu za kahawa zilikuwa tofauti kabisa. Baada ya kuwekwa kwenye maji ya moto, ziliyabadilisha maji yenyewe.
“Wewe ni kipi kati ya hivyo?” bibi alimuuliza mjukuu wake. “Masaibu na mashaka yanapobisha hodi mlangoni kwako, unaitikia vipi?
Je, wewe ni karoti, yai au mbegu ya kahawa?
Fikiria hivi: Je, mimi ni nani? Je, mimi ni karoti inayoonekana kuwa imara lakini inapokumbwa na mashaka inakuwa tofauti? Je, ninafifia, ninalainika na kupoteza nguvu zangu?
Je, mimi ni yai ambalo huanza kwa kuwa na moyo laini, lakini hubadilika joto linalopanda? Je, nina moyo wa kimiminika, lakini baada ya masaibu au mashaka ya kiuchumi au mitihani mingine ninakuwa mgumu na imara?
Je, gamba langu la nje linaonekana kuwa tete lakini kwa ndani nina moyo imara na madhubuti?
Au mimi ni kama mbegu ya kahawa? Mbegu hiyo hubadilika inapokutana na maji ya moto, mazingira yaleyale yanayoleta maumivu… maji yanapopata moto, hutoa harufu nzuri na ladha maridhawa. Kama wewe ni kama kahawa, mambo yanapokuwa magumu, unaimarika na kuibadilisha hali inayokuzunguka. Nyakati zinapokuwa ngumu na mitihani kuwa mikubwa, je unajibadilisha kwenda kwenye hali nyingine?
Unayakabili vipi magumu na mashaka yanayojitokeza? Je, wewe ni karoti, yai au mbegu ya kahawa?
https://www.facebook.com/allaboutrelationshipandlife/

Chapisha Maoni

0 Maoni