Hassan alikua akiendesha gari taratibu sana, alikua na huzuni, akiwa kimya muda wote akijikaza ili asilie mbele ya Mama yake. “Kwahiyo umeamua nini?” Mama yake alimuuliza, alinyanyua uso wake na kumgeukia kidogo kisha akarudisha macho kwenye usukani. “Kuhusu nini Mama?” Aliuliza kwa sauti ya upole huku akigeuka tena kumuangalia Mama yake.
“Kuhusu nini? Si mkeo, inamaana hutaki tena mtoto! Hyu ni mtoto wa tatu anafia tumboni unafikiri atazaa tena huyo mwanamke?” Mama yake aliongea kwa sauti ya juu iliyojaa msisitizo. Inaonekana ni kitu alichokua akikiwaza kwa muda mrefu. Hassan alishindwa hata chakuongea, hakujua amjibu nini kwani ni swali ambalo hakulitegemea hasa kwa kipindi kile.
Ilikua ni siku ya pili mke wake akiwa Hpspitalini, akijaribu kujifungua mara tu baada ya kuambiwa kua moto wake amefia tumboni. Ndiyo alikua anasubiri kupata uchungu ili ajifungue maiti. Baada ya kubeba mimba ya miezi nane safari hii akiwa makini sana, akiwa ameenda Kiliniki ya kawaida tu aliambiwa kua mtoto amefia tumboni.
Hakuwa anumwa wala kujisikia chochote. Hassan ambaye alikua ameongozana na mke wake Kiliniki alikua mwanaume, alimbembeleza na kumpa moyo lakini Halima alizimia mara nne baada ya kupata zile habari. Alihamishiwa Hospitali binafsi ili kuangaliwa ziadi, akisubiriwa ajifungue kwa njia ya kawaida. Hakua mtoto wa kwanza na lile halikua tukio la kwanza bali la nne.
Mimba yake ya kwanza mwaka mmoja tu baada ya kuolewa ilitoka ikiwa na miezi miwili, baada ya hapo alipata ujauzito mwingine na ilipofika miezi saba mtoto alifia tumboni, aligoma kutoka na kulazimika kufanyiwa upasuaji. Mwaka uliofuata alipata mimba nyingine, ilipofika miezi saba mtoto alifia tena tumboni na kama ile ya kwanza haikutoka kwa njia ya kawaida bali kwa kisu.
Hii ilikua ni mimba ya nne na mtoto wa tatu kufia tumboni, madaktari walisita kumpasua tena kwani alikua hana hata mtoto hata mmoja. Hassan ambaye ni mtoto wa kwanza kwao alikua ndani ya ndoa miaka sita bila kupata mtoto, wadogo zake waliooa nyuma yake walikua na watoto tayari hivyo baada ya lile tukio Mama yake aliona kama mkwewe ana matatizo.
“Mama mke wangu bado yuko Hospitalini, hata kujifungua bado nianze kuwaza kuhusu mtoto?” Aliuliza kwa sauti ya unyonge, alishindwa kujizuia machozi yalimtoka, alinyanya ua bega lake la kulia na kujifuta, Mama yake alimuangalia kwa huruma kidogo lakini hakukoma aliendelea. “Tatizo ni mke wako, hawezi kubeba mimba yule bora uoe mwingine Dini inaruhusu!”
Hassan alinyamaza kimya, ndani alikua amepandwa na hasira anaungua kabisa, lakini alikumbuka yule ni Mama yake hivyo asingeweza kumfanya chochote. Aliendesha gari mpaka nyumbani. Aliingia chumbani kumchukulia mkewe nguo za kubadilisha, tayari chakula kilishaandaliwa lakini hakutaka kukaa kula, alichukua chakula cha mkewe na kuondoka.
Tayari Mama yake alishamtia nyongo na alijua kabisa akikaa naye pale uvumilivu utamshinda atamkosea heshima. Alirudi Hospitalini, mkewe alikua ameshaamka, alikaa pembeni yake na kumkumbatia, alimuambia usiwe na wasiwasi kila kitu kitakua sawa. Mkewe alishalia mpaka machozi yakaisha, alimuangalia mumewe na kumuonea huruma.
“Sasa, ndugu zako watasemaje mume wangu, natamani nikuzalie na wewe uitwe Baba, tumuombe Mungu nijifungue salama nikutafutie mtoto mwingine...” aliongea akionyesha kumuonea huruma mume wake. Hassan alimuangalia mkewe huku machozi yakimtoka alimkumbatia na kumuambia. “Usijali kuhusu ndugu zangu, tuombe mungu upone hayo mambo ya watoto ni ya baadaye sasa hivi tupiganie afya yako kwanza.”
Mkewe alijaribu kuongea lakini alimuambia anyamaze asiwaze sana. Walikaa Hospitalini wiki moja bila kujifungua, walimuwekea maji ya uchungu lakini wapi hakuna kitu. Walitaka kumfanyia oparesheni lakini Halima alikataa, alijua fika kama akiruhusu apasuliwe tena itakua ngumu kupata mtoto karibuni, angetakiwa kusubiri sana kabla ya kupata mimba nyingine na yeye hakutaka hivyo.
Aliruhusiwa kuondoka, alikaa nyumbani mwezi mzima na mimba yake, mtoto akiwa tayari ashafia tumboni lakini bado hakujifungua, alianza kuumwa tumbo wakalazimika kumfanyia upasuaji. Hili lilikua pigo jingine kwani baada ya hapo aliporudi nyumbani Mama mkwe alianza kuwa Pilipili, kila siku akitaka mtoto wake aoe mke mwingine kwani yule hata zaa tena.
Hassan alivumilia mpaka yakamfika shingoni, Mama yake ambaye alikuja pale kumsaidia mkewe katika alikataa kuondoka mpaka mwanae aoe mke mwingine. Halima alimruhusu akimsitiza amsikilize Mama yake kwani yeye haoni kama anaweza kumpa mtoto,Hassan hakua tayari kwa hilo, alisisitiza kama Mungu angetaka kumpa mtoto angempa tu kwa wakati wake.
Siku moja Hassan alimfuata Mama yake, alimuambia kamsikia na yeye anatamani sana mtoto lakini hawezi kuolea pale mjini hivyo kama angemtafutia mwanamke kijijini akamzalisha huko ndiyo akamuambia mkewe basi ingekua rahisi. Mama yake alifurahi sana alianza kuwaza kurudi Kijijini, alijiandaa kuondoka na Hassan alimuaga mkewe kuwa anmpelaka Mama kijijini.
Walienda walipofika huko siku iliyofuata Mama yake alianza kumtajia majina ya mabinti ambao anaweza kuoa pale Kijijini, Hassan alimuambia “Mama sikuja kuoa, nimekuja kukurudisha nyumbani kwani nilishaona kama nikiendelea kuishi nawewe tungegombana na ningekukosea heshima. Sina mpango wa kuoa mwanamke mwingine na kama Mungu hataki nipate mtoto kwa mke wangu basi sihitaji mtoto kabisa…”
Mama yake alishangaa, huku akiwa amekasirika alimuambia “Labda kama mimi si Mama yako utaoa, nimekuweka tumboni miezi tisa autaoa tu na wajukuu utaniletea na kama umeona mkeo ndiyo wa muhimu kiasi cha kunidharau mimi Mama yako basi ukiondoka hapa usikanyage tena, ondoka ukijua kuwa mimi si Mama yako tena na hata nikifa usije kunizika…”
Hassan alitabasmu kisha akamuambia “Mama, wewe hata ufanye nini ni Mama yangu tu na kama unataka kuninyima radhi kisa sitaki kumuacha mke wangu basi ninyime tu. Ukifa nitakuja kukuzika kama utafufuka ufufuke na wewe ni Mama yangu nitaendelea kukuhudumia nitakutumia pesa kama hutazitumia basi lakini mke wangu sitamuacha na sioi mwingine…”
Aliongea taratibu kisha akamuaga Mama yake na kuondoka, Baba yake alishafariki. Alirudi kwa mkewe na maishja yaliendelea, Mama yake alikua hapokei simu zake lakini kila mwezi Hassan aliendelea kumtumia pesa za matumizi. Alimuambia mke wake hataki tena kusikia suala la mtoto na wala wasijaribu tena kumtafuta.
Lakini miaka miwili baadaye mkewe alipata mimba nyingine, hawakumambia mtu yeyote kwani walijua inaweza isifike popote. Lakini wakiwa hawaamini miezi tisa ilifika na mkewe alijifungua mapacha watatu tena kwa njia ya kawaida kabisa. Hakuna aliyeamini hawakutaka kumuambia mtu mpaka watoto wawe wakubwa wakubwa.
Hata ndugu zao hawakuwaambia, watoto walipofikisha miezi sita ndipo walipoamini kuwa kweli ni wakwao, waliwaambia ndugu na kuwapeleka Kijijini. Mama yao alishangaa sana, alilia huku akiomba msamaha, hakuamini kilichotokea. Kila siku alikua akimuomba Mungu asife kabla ya kuwaona wajukuu wa mtoto wake wa kwanza na Mungu alijibu maombi yake.
***MWISHO;
0 Maoni