Mtu mmoja aliniuliza ni kwanini ndugu wa mume wana gubu hivyo? Nilimuangalia kisha nikamuambia twenda nikuonyeshe, tulikua tumekaa sehemu, niliangalia kulikua na mwiba nikamuambia vua kiatu chako.
Alivua na niliuchomba ule mwiba mpaka ukatokezea juu, kisha nikamuambia vaa, alijaribu kuvaa lakini kabla ya kuufikisha mguu ndani aliutoa kwani ule mwiba ulitaka kumchoma.
Alipokivua nikachukua mwiba uleule kisha nikauchoma kwenye kiatu kingine nikamuambia usikivae. Hakukivaa na hakuchomwa na mwiba, hakunielewa mfano wangu nikamuambia kuwa tatizo sio ndugu wa mume bali ni ndugu wote.
Kila familia ina changamoto zake, watu hutumia miaka kadhaa kuzoeana, kujuana tabia na kuchukuliana poa. Ukiangalia katika familia yako kuna ndugu mkorofi, hamuelewani lakini mnaishi kwakua ni ndugu na mnavumilia.
Mama yako inawezekana ana gubu, anaongea sana na unamvumilia kwakua ni Mama yako. Kila familia ipo hivyo, ina matatizo yake, kila familia ni sawa na kiatu kina mwiba wake.
Sasa kinachotokea mpaka familia ya mwanaume kuonekana ina gubu nikwakua mwanamke akiolewa anaenda kuishi kwa mume na si mwanaume anaenda kuishi kwa mke. Kwamba anaenda kuwa mgeni, katika familia ambayo ina miba yake mingi tu, miiba ambayo hajaizoea na hajajua namna ya kuishi nayo.
Hii haimaanishi familia yake haina tatizo hapana inayo mengi tu, lakini nikwavile tu mwanaume haendi kuishi ukweni, hakutani na ile mikiki mikiki ya kila siku. Ukitaka kujua familia zote zina gubu basi hembu angalia familia ambayo mwanaume anaishi ukweni.
Huyo ndiyo anaisoma na kundika namba. Kwamaana hiyo basi unapoolewa unapaswa kujua kuwa kuna uwezekano wa kukutana na miba, ingawa si lazima lakini ipo tu kwenye kiatu hivyo jiandae kuishi nayo vizuri, kuwavumilia na kubwa kabisa kuwapuuza.
Usichukulie kila kitu siriasi, wapuuze kwa mambo mengine, wakuone mjinga huku ukijua kuwa hawataishi na wewe milele kwani nao watakua na familia zo watenda kukutana na viatu vyao na miba yao.

0 Maoni