
We ndio wangu wathamani, niliyekupenda zamani,
Moyoni nitakuthamini, kwa siri hata hadharani,
Usiniache peke yangu jangwani, nilaze kwako kifuani.
Jina langu Kadala, thamani yangu Jalala.
Njoo nikupe mambo ya pwani, japo kwenu uchagani,
Njoo nikupe mambo ya pwani, japo kwenu uchagani,
Nipeleke kwenu nyumbani, tufunge ndoa maishani,
Mtapanga sana foleni, mi napelekwa ukweni,
Jina langu kadala, thamani yangu Jalala.
Kizuri hakikai mdomoni, lakini midomo fungeni,
Wambea wote taabani, maji yamewakwama shingoni,
Maneno yamekwisha mdomoni, kamasi zawatoka puani,
Jina langu kadala, thamani yangu jalala.
Mimi ndio mtoto wa pwani,niliyefunzwa unyagoni,
Mume akitoka sokoni, nampokea vya mkononi,
Nampa busu shavuni, namshika mkono chumbani,
Jina langu kadala, thamani yangu jalala.
Utamu wangu jikoni, mume hukomba sahani,
Wala sio uchwani, ni mapenzi tu jamani,
Nampa vyote vya ndani, asitoroke nyumbani
Jina langu Kadala, thamani yangu jalala.
Hasira zangu hazioni, ninapokwazika moyoni,
Namnong’oneza sikioni,aliyoyatenda hayafai,
Mapenzi wala si usomi, ni utundu tu wa ndani,
Jina langu Kadala, thamani yangu jalala.
Makosa yake ya ndani, nayahifadhi moyoni,
Kwa jirani siyasemi, sio heshima ndoani,
Mwanamke kutunza siri, sio kubwabwaja hadharani,
Jina langu kadala , thamani yangu jalala.
Mume wangu mtanashati, kwa juhudi zangu za usafi,
Nyumbani kwangu hapanuki, ndio maana habanduki,
Udi na mengine marashi,napulizia bila wasi wasi,
Jina langu kadala, thamani yangu jalala.
Mkwe namuweka safi, kwa mavazi wala hazeeki,
Amenizalia askari, jemedali aongoza safari,
Namfanya wangu rafiki, unafiki nauweka mbali,
Jina langu kadala, thamani yangu jalala.
Nafunga yangu kauli, wala sijipambi kwa mazuri,
Yote niliyofanya kwa uzuri,naonekana jeuri,
Namshukuru rasuli , nakumuachia jalali,
Jina langu kadala, thamani yangu jalala.
0 Maoni