NINI CHA KUFANYA UNAPOMFUMANIA MUME WAKO MARA KWA MARA NA HATAKI KUBADILIKA!



Image may contain: 1 person, smiling

Hili ni swali ambalo naulizwa kila siku, ingawa nimekua nikimjibu mtu mmoja mmoja lakini nimeona niandike hii Makala ili wengine nao wafaidi hata wale ambao hawakuniomba ushauri. Ninaposema kumfumania mume wako namaanisha mume na simaanishi mpenzi wa kawaida, ingawa mbinu hizi unaweza kuzitumia katika mpenzi wa kawaida lakini ningependa ufanye hivi kama kakuoa ni mume wako au hata mnaishi pamoja na mna watoto.
Ninaposeama unamfumania mara kwa mara na maanisha kua kama umemfumania mume wako zaidi ya mara mbili, iwe ni kwa kumkuta moja kwa moja au kwa kuona meseji ambazo zinakuambia kua anachepuka basi Makala hii inakuhusu. Anaweza kuwa kila ukimfumania anaomba msamaha, au haombi lakini unaamua kumsamehe na kudhani kua atabadilika ila baada ya siku kadhaa anarudia hali hiyo hiyo.
Inawezekana ushawaambia mpaka ndugu, mmeshajaribu kusuluhisha lakini bado, unaumia na hujui cha kufanya. Anaweza kuwa anachepuka na wanawake wengiwengi au mmoja, kazaa naye au anahudumia na hata kumpenda kuliko anavyokupenda wewe. Kama uko kwenye hali hii basi haya ndiyo mambo ambayo unaweza kuyafanya na yakakusaidia, anaweza asibadilike lakini yatakupunguzia machungu na kukutengenezea maisha yako.
(1) Amua Kujilinda; Mwanaume anapochepuka mara mbili tatu huanza kuzoea, huona kama kile kitu anachofanya ni cha kawaida na wakati mwingine haoni hata haja ya kuomba msamaha. Kama ni hivyo basi kama mwanamke unatakiwa kujua namna ya kujilinda, kwamba anapochepuka sio kama tu anakuumiza hisia zako lakini siku hizi kuna magonjwa, kuvumilia kulikokua kunafanywa na Mama zetu ilikua ni kuvumilia kuumizwa hisia.
Lakini kwa sasa huwezi kuvumilia kuambukizwa magonjwa, kwamba hata kama unampenda vipi, unauvumilivu kiasi gani unasali na kumuomba Mungu haiwezi kusiadia kama hutajilinda, kutokana na umalaya wake kama akiambukizwa magonjwa basi jua na wewe utaambukizwa. Kwa maana hiyo, ingawa najua ni ngumu lakini hembu anza kwa kujilinda, hapa kuna mambo mawili ambayo unaweza kufanya, jambo la kwanza ni kujilinda kwa kuondoka.
Kusema kwamba pamoja nakua nampenda mume wangu, naipenda ndoa lakini tabia yake imenichosha, habadiliki hivyo unaamua kuondoka na kuanza maisha yako bile yeye. Huo ndiyo ushauri wangu wakwanza, lakini pia najua ni wanawake wachache sana ambao wanaweza kuondoka, wengi bado mtachagua kuvumilia, kuna sababu nyingi zinawafanya hivyo na sitaki kuzizungumzia hapa.
Kama wewe mume wako anachepuka mara kwa mara na unajua wazi huwezi kuondoka basi ushauri wangu ni kwa wewe kujilinda kwa namna ya pili ambayo ni kwa kutumia kinga. Angalau dai kutumia Condom. Kwamba umemfumania mara nyingi tena na wanawake wengi na unajua huwezi kuondoka. Hembu kua na ujasiri hata wakusema kua mume wangu pamoja na yote lakini huugusi mwili wangu bila kinga kwani sitaki kuambukizwa magonjwa.
Kwakumuambia mtumie kinga mbali na kua unajilinda na magonjwa lakini ni kama unampa ujumbe kua umechoka hiyo hali yake, unamuambia kua unajipenda na hauko tayari kuendelea kuhatarisha maisha yako kwaajili yake. Narudia inaweza kuwa ngumu lakini tengeneza huo ujasiri, hata kama akitishia kua kama hutaki kavukavu basi anarudia kuchepuka basi simamia msimamo wako, nilazima ajue nawewe umechoka na hiyo hali.
(2) Anza Kujiweka Huru Kiuchumi; Unapomfumania mwanaume mara nyingi na wanawake tofauti ni kama anakupa ujumbe kua ninaweza kukuacha na kwenda kwingine. Anakuambia kua hauko peke yako hivyo hata kama utaamua kuvumilia kuendelea kuishi naye ni lazima ujue kua maisha si mapenzi tu, kuna kitu kingine cha zaidi. Kwamba wanawake wengi hunyanyasika kwakua hawako huru kikipato na hata sikwakua si wazuri au wanaume wanachepuka!
Kwanza nikwakua wengi ni Mama wa nyumbani au hata wale wanaofanya kazi wanakua na kipato kidogo kuweza kuishi pake yao. Kama mume wako anachepuka ni lazima sasa uwaze kuachika, uwaze kuwa hivi akiniacha leo nitaenda wapi? Sasa kama unafanya kazi basi hembu waza hii kazi inaweza kunifanya kujitegemea kikipato, je naweza kuhudumia wanangu kama akinitelekeza na hii kazi.
Kama jibu ni hapana nilazima uanze kutengeneza kipato cha ziada, nilazima uanze kuweka akiba na hapa kama ni kumchuna huyo mwanaume na kuwekeza kivyako anza kuwekeza. Huyo mwanaume huko anakokwenda hapewi mapenzi bure, kwa namna flani atakua anahudumia hivyo anawekeza pesa zake huko hembu na wewe anza kuwaza namna ya kuwekeza. Kama alikukataza kufanya kazi basi anza kutafuta kazi yoyote ile.
Kama ni biashara basi anza kutafuta biashara ya kufanya na kama akitaka kukukataza muambie kabisa bila kuficha kuwa umeshachepuka hivyo siwezi kuvumilia kukaa hapa nyumbani kusubiri uniache na kuninyanyasa na watoto. Muambie kama umeweza kunisaliti naamini unaweza kuniacha hivyo mume wangu nakupenda sana lakini najiandaa ili kama ukiniacha basi niwe na pakushika na si kwenda kuwa mzigo kwa ndugu.
(3) Acha Kumfuatilia Na Fuatilia Anapopeleka Pesa; Kwa wanawake wengi anapomfumania mume wake anaona ni wakati sasa wa kumchunga, kufuatilia michepuko yake, kuipigia simu, kuitukana na kuiambia achana na mume wangu. Hapana acha huo ujinga wa kujidhalilisha na kujipotezea muda, hataachana na mumeo kwani hajali hisia zako na hata akiachana mumeo kama ushamfumania mara mbili tatu jua kua mumo ni Malaya hivyo hata akimuacha huyo unayempigia simu atatafuta mwingine.
Mfuatilie mume wako lakini si kujua kama anaendelea kuchepuka au la, kuchepuka bado anachepuka ila hembu fuatilia pesa zake, je anafanya kitu cha maendeleo, anamhudumiaje huyo mwanamke. Nakuambia hivi kwakua kuna wanawake wao ni kufuatilia tu simu kumbe mume anajenga sehemu, anaujengea mchepuko, wewe unaishi kushida, unabana matumizi kumbe kuna sehemu ambayo anapeleka pesa zake.
Fuatilia na jua mali zake zote, hata kama hamgombani lakini jua kua mumeo ana nini na nini? Kama nilivyokuambia awali kua kama kakusaliti anaweza kukutelekeza, kwa maana hiyo basi hata kama akikutelekeza au akitaka kukuacha basi unajua ana mali gani na pale akikuambia huondoki na chochote unamuambia hapana tutagawana kila kitu! Kwa kifupi acha kupelekwa pelekwa na kwa kutokujua mali zake, zijue na jiandae kwa kila kitu.
(4) Acha kunyenyekea na anza kujipenda; Hii ndiyo sababu kubwa mwanaume wako anazidi kuchepuka kila siku tena bila kificho, ulipomfumania mara ya kwanza ulimsamehe, ya pili ukamsamehe ukazidisha mapenzi na kumnyenyekea. Unapomnyanyekea mwanaume ambaye kakusaliti, huonekani hata kukasirika ni kama unamuambia mume wangu ulichokifanya ni sawa na endelea mimi ndiyo nilifanya makosa ya kukufumania na kupekua simu yako.
Hawezi kuacha kwani anaona kama hatendi kosa, hivyo kama unamfumania kila siku na ndiyo umemaua kubaki huwezi kumuacha hembu anza kujipenda, badala ya kuangalia yeye anataka nini hembu angalia wewe unataka nini? Jifunze kutengeneza furaha yako mwenyewe! Sisemi uwe kiburi au usimjali au uwe mtu wa kununa kila mara, hapana ila hembu kua mtu wa furaha, kuna mambo yanayokupa furaha, kuna mambo ulikua unatamani kuyafanya hembu jifanyie.
Acha kukaa ndani kuomboleza, kujiona kama hunathamani, kuona kama maisha ndiyo yamefikia mwisho hapana. Mume wako anafuraha na mambo anayoyafanya huko, hembu na wewe anza kuwa na furaha, fanya mambo ambayo hukupa furaha. Ukifanya hivi kwanza utakua na furaha lakini pili utampa ujumbe kua maisha yanaweza kuendelea bila yeye, unapokua unalia kila siku unazidi kumpa kiburi kuwa anaweza kukutawala na kukufanyia chochote kile kwani huna maisha.
(5) Acha Kuwa Baba Wa Familia Rudi Kuwa Mama; Kuchepuka kunahitaji hela, ni wanawake wachache sana ambao watasikia kua flani ameoa halafu wakawa na mahusiano ambayo hayagusi hela. Kwa maana hiyo basi kama mume wako anachepuka moja kwa moja atakua anahonga na kama anahonga basi moja kwa moja atakua akipunguza matumizi hapo nyumbani na kukuachia majukumu yake yote.
Hapana, ukishamfumania mume wako acha kubeba majukumu yake na kama habebi basi yabaki hivyo hivyo. Inawezekana umeajiriwa au unakabiashara kako hivyo anajua kua hata asipotoa matumizi atarudi nyumbani na kukuta chakula, hapana. Kama hatoi matumizi akirudi nyumbani basi akute ushawapikia watoto chakula kimeisha, kama akirudi akute umeme hakuna na kama hatalipa ada ya watoto basi wabaki hapo nyumbani.
Amua kabisa kuwa Mama, pesa zako anza kuwekeza katika mambo yako binafsi, wekeza vitu kwa majina ya watoto wewe ukiwa kama msimamizi wao. Hakikisha watoto wanapata chakula na matibabu ila mambo mengine muachie, hata ada muachie na kama hatalipa awaone watoto hawaendi shule, kwa kifupi asijue kua kama akikutelekezea familia utalea hapana nilazima umpunguzie hela yake ya kuhonga sio wewe unahangaika na familia yeye anahonga!
(6) Weka Malengo Ya Maisha Yako; Unataka nini katika maisha yako, utaishi katika hali hiyo mpaka lini? Najua ndoa ni ya watu wawili mlipaswa kuwaza na kuwa na malengo ya aina moja. Lakini kuna wakati unafika dada zangu nilazima mjiangalie nyinyi, kama mwanamke uwe na malengo yako, mambo ambayo wewe unataka kuyafanikisha wewe kama wewe. Acha kuwa mtu wa kukaa ndani na kulia, kuwaza kuhusu mume wako na kuona kama maisha yameisha.
Ulikua na maisha kabla yake na utakua na maisha baada yake. Hata kama ni mvumilivu kiasi gani nina uhakika kuna wakati utachoka, swali ni je ukichoka utafanya nini? Hembu jiulize kama akiendelea kuwa hivyo miaka kumi utafanya nini? Je utaendelea kuvimilia ukilia, utaondoka au utatengeneza maisha yako binafsi na kutengeneza furaha ambayo haimhusu yeye. Hembu kama uko katika hali hii kua mbinafsi kidogo na anza kuwaza kama haujaolewa.
Hata kama kwako bado ni ngumu kuondoka, kama ushajikatia tamaa na kusema liwalo na lile lakini hata kama hutaondoka wewe anaweza kukuacha je utafanya nini? Pamoja na mambo yote niliyoyazungumza hapo juu hembu sasa anza kuweka malengo yako binafsi, kuwaza wewe kama wewe ili hata kama hatabadilika lakini uwe na mipango yako mwenyewe na si kusubiri uachwe huna uelekeo ndiyo uanze kuhangaika hangaika.

Chapisha Maoni

0 Maoni