KUPENDANA pekee hakutoshi kufanya mahusiano yenu yawe ya furaha na amani. Mbali na kupendana na kuwa pamoja, kuna mambo mengi ya msingi yanatakiwa kufanywa. Leo sitozungumzia sana masuala ya uaminifu. Hiyo ni mada ambayo inazungumzwa na wengi na tumekuwa tukiisema mara kwa mara.
Kabla hatujaenda mbali, nakuuliza. Unafanya nini kumfanya mwenzako awe na furaha na amani? Unafanya nini mwenzako azidi kukuona wa thamani na maana katika maisha yake?
Binadamu ni kiumbe anayechoka haraka. Njia pekee ya kumfanya asichoke kwako na kwa matendo yako ni kuepuka kumfanyia mambo yale yale kila siku.
Mapenzi ni mchezo wa akili(game of mind). Ili mwenzako akuone wa thamani na bora ni lazima ujue kucheza na akili yake.
Anza kujiangalia katika mavazi yako. kila siku umekuwa mtu wa kuvaa yale yale mkiwa faragha pamoja( kwa wanawake)? Acha kuishi kwa mazoea. Ili mwenzako akuone mpya inabidi uwe unabadilika badilika katika suala la mavazi muwapo pamoja. Aina moja ya mavazi, tena yale yasiomsisimua na kumpendeza mwenzio sio tu hali hiyo itafanya asiwe na shauku ya kuwa na wewe pamoja ila pia itamfanya atamani vingine.
Kama tulivyosema hapo awali, akili ya binadamu huwa inachoshwa na vitu visivyobadilika, vitu ambavyo kila siku viko vile vile na vinafanywa katika
mtindo ule ule( monotonous), huwa havileti shauku kwa muhusika.
Hata kama kitu kikiwa kizuri namna gani ila kama kinakuja katika mtindo ule ule kila siku, huwa kinachosha na kukosa mvuto stahili. Huu ndiyo ukweli. Ndiyo maana mtu anaweza kutumia pesa nyingi sana kununua nguo mpya hata Kama katika kabati lake zipo nguo nzuri zaidi ya ile anayotaka kununua. Hali hii inasababishwa na hali ya binadamu kupenda vitu vipya. Katika akili ya kibinadamu upya ndiyo uzuri. Ili kumfanya mwenzako aweze kubabaika na wewe uwe unatinga mavazi tofauti muwapo faragha. Usikariri.
Pia katika suala la maisha na mambo mengine ya ndani uko vipi? Wanaume wengi wamepoteza hamasa kwa wake zao kutokana na namna yao ya kuishi. Hata wakiwa wanachati na wake zao hawasisimui wala hawawafanyi wasisimkwe. Ndugu zangu, mapenzi ni suala la ubunifu na ujanja.
Ongea na mpenzi wako katika mazungumzo na mijadala tofauti. Sio kila siku ukichati naye ni suala la kuulizia hali ya watoto, salamu tu na mambo mengine ya kifamilia. Taniana na mpenzi wako. Jadili masuala mengine anayopenda na kufurahisha.
Wanaume wengine wanachosha sana. Eti ukimwambia kwanini huwi na stori ama na utani na mkeo, anajibu kwamba yeye mwanaume atakuwa na stori gani na mkewe! Wao wanachojua mwanamke rafiki yake ni mwanamke tu. fikra za hovyo kabisa hizi.
Tathimini zinaonesha mwanaume ambaye anamfanya mkewe kuwa rafiki yake, ana uwezo wa kuifanya
ndoa yake kuwa ya amani na raha. Hii inasababishwa na utani pamoja na stori ambazo watakuwa wanapiga.
Utani na stori za mara kwa mara zinawajenga wahusika kuwa huru kwa kila mmoja pamoja na kusema yale wanayotamani kufanya ama kufanyiwa. Pia utani na stori za mara kwa mara huwafanya wahusika wawe na uwanja mpana wa kujadili masuala na changamoto zao. Wewe unaishi vipi na mpenzi wako?
Ili mpenzi wako afurahie maisha na wewe, inabidi awe na raha na amani akikuona ama akikukumbuka. Na hili suala ni gumu kuwezekana kama muhusika anakuchukulia kama ‘jitu serious sana’.
Mahusiano mengi yanayokosa mvuto na hatimaye kuvunjika ni yale ambayo wahusika wameoana ila wanaishi kama wako mkutanoni. Yaani wako serious sana, hakuna utani, hakuna mada tofauti tofauti baina yao zaidi ya masuala ya familia tu. Hii kitu inapunguza sana mvuto na hamasa ya maisha ya wawili.
Wengi wanakosea pale wanapodhani mazungumzo muhimu ndiyo kitu pekee cha kuzungumza na wandani wao. Makosa makubwa haya.
Mazungumzo ya kawaida, yale yanayoonekana yakijinga na yenye kufurahisha ndiyo yenye kujenga zaidi amani na mshikamano baina ya wahusika kuliko hata hayo mengine.
Wanaume inabidi wabadilike kudhani kuwa eti kuwa na utani na mpenzi wako ndiyo chanzo cha dharau na kuonekana sio lolote. Sio kweli hata kidogo. Kuwa na utani na mijadala tofauti na mpenzi wako ndiyo chanzo cha mahusiano yenu kudumu na kuleta amani.
Ili mpenzi wako azidiwe na mapenzi juu yako inabidi katika akili yake akuone katika namna nyingi. Akuone mpenzi, rafiki, mtani na hata mpinzani wake katika baadhi ya masuala. Kwa kuwa hivi mpenzi wako atakuwa anakufikiria na kukuwaza muda mwingi. Unajua faida ya mwenzako kukufikiria na kukuwaza muda mwingi? Ni yeye kutamani kuwa karibua na wewe. Sasa hasara iko wapi hapa?
Mwenzako akikufikiria muda mwingi maana yake umetawala maisha yake. Na kama umetawala maisha yake, ni kwanini afungue mlango kwa ajili ya mtu mwingine?
Kuwa mbunifu katika maisha yako ili mwenzako ajisikie fahari na amani kuwa na wewe. Usiwe aina ya mtu ambaye unamfanya mwenzako ajione mpweke hali tayari yuko na wewe katika maisha yake.
Mapenzi sio kuambiana tu jinsi mnavyopendana na kuheshimina. Ila ni jumla ya matendo yote mazuri ya kufurahisha na kutiana hamasa. Kwako hali ikoje?
Kuanzia saa chunguza aina ya maisha ya kimahusiano uliopo. Je maisha yako hayo yanamfanya muhusika kujidai na kujiona wa fahari kuwa katika maisha yako? Maisha yako hayo, yanamfanya mwenzako kujivunia kuwa katika maisha yako? Majibu ya maswali hayo yatakupa uelekeo wa aina ya mahusiano yako na njia gani yanaenda.
Mwandishi wa makala hii ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia( Psychoanalyst)
https://www.facebook.com/allaboutrelationshipandlife/

0 Maoni