HUNA MAONGEZI YA KUMWAMBIA MPENZI WAKO, KUWA HIVI

Image result for mahusiano


TUMEUMBWA tofauti. Wapo wenye uwezo wa kuongea sana na pia wapo wenye kutumia muda mwingi kuwa kimya. Si kama wanatafakari sana, hapana.
Ila ni mazoea yao kukaa kimya tu. Hii haimaanishi hawajui mambo mengi, la. Ila hulka zao ni kukaa kimya na kusikiliza wengine.
Unaweza kuongea jambo analolijua sana ila badala ya yeye kuliendeleza ama kulishabikia, anaweza kukusikiliza kwa makini na kuishia kutabasamu tu. Ndivyo binadamu tulivyo.
Kuna tatizo fulani katika hili. Wapo wanaoteseka zaidi ya mazoea ya kawaida ya kukaa kimya. Ndiyo, kukaa kimya ni hulka ya mtu, na kwa namna fulani huwezi kumlazimisha mtu kuwa muongeaji hata kama sio.
Na inapotokea unamlazimisha, mbali na kumfanya afanye kitu ambacho hakipendi, ila pia unamlazimisha kusema kitu ambacho hana. Na kwa namna hii si ajabu akasema neno baya au lisilo na mvuto katika masikio ya wasikilizaji.
Ila mbali na ukweli huo, watu wanapenda wakiwa na wenzi wao wapate maneno ya kuongea. Hapa kuna neno zaidi. Hapa wapo hata wale waongeaji ila wakati mwingine wakiwa na wapenzi wao wanajikuta hawana maneno ya kuongea.
Mifano ipo. Na wengi wamewahi kunifuata wakiwa na tatizo hilo. Japo kuna njia nyingi za kufanya, ila hapa nitapenda tuangalie chache sana.
Kama wewe ni miongoni mwa wale wenye kupenda kuongea na wapenzi wao ila kila mnapokutana maneno  hupaa, usijali.
Kwanza, jambo unalotakiwa kulifanya ni kutolichukulia suala la maongezi yenu kuwa ni serious sana. Kwa kuwa ni mpenzi wako na maongezi ambayo unapenda kufanya naye ni ya kawaida, ‘relax’. Tena hata ukiwa peke yako acha kujisumbua kwa kupanga maongezi ya kufanya naye. Kuna baadhi ya mambo huja yenyewe tu ikiwa unajua ni njia gani za kufanya.
Ukikutana naye, acha kutaka kuongea mambo ambayo huna ujuzi nayo. Mara nyingi watu wanakosea pale wanapokuwa na mpenzi wake na kutaka kujifanya anajua jambo fulani hali ya kuwa hujui. Hali kama hii inakufanya ukose hali ya kujiamini na matokeo  yake unaona maongezi husika ni kama adhabu kwako.Kwani nani kasema kuwa maongezi ya wapendanao ni magumu na yenye kutumia akili nyingi sana? Acha hizo. Zungumza naye kuhusiana na mambo unayoyajua. Mambo kama filamu, muziki hata na mazingira mnayoishi yatafaa zaidi.
Na ili kumfurahisha zaidi, penda kumsoma mwenzako anapenda nini? Kama ni mtu wa muziki, penda kuzungumzia maongezi hayo na pia usitake muda wote kuzungumza wewe tu. Hapana. Mpe na yeye muda. Suala la kumpa muda mbali na kumfanya afurahie mazungumzo yenu, ila pia nukta ya neno lake itakuwa inakupa na wewe cha kusema.
Na kitu kingine, kama unajiona huna kabisa hata namna ya kuanza kuzungumza. Penda kusoma vitabu, magazeti na kusikiliza redio. Kwa kufanya hivyo, utajikuta unajua mambo mengi, hali itakayokujengea shauku ya kutaka kuzungumza.
Huna haja ya kuumiza kichwa kutaka kujua nini unatakiwa kuzungumza. Relax, kisha zungumza kitu unachokijua. Sheria ya mazungumzo, ukianza neno wewe, na yeye lake mtajikuta mna muda mwingi wa kuzungumza bila hata kuchoshana. Anzisha mazungumzo uone.


https://www.facebook.com/allaboutrelationshipandlife/

Chapisha Maoni

0 Maoni