
Katika juhudi zetu za kutafuta mkwanja (Fedha) mimi na mume wangu tukakubaliana tutafute house girl ili atusaidia kukaa na mtoto wetu ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli nyingine za usafi kwa ujumla pale nyumbani.
Baada ya kuhangaika sana, maana siku hizi ma house girl wamekuwa adimu sana hapa jijini Dar es salaam, kutokana na juhudi za serikali yetu kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata elimu.Tofauti na zamani ambapo ilikuwa kila mwisho wa mwaka watoto hasa wa kike wanaomaliza darasa la saba wanaletwa mjini kutafutiwa kazi za ndani, siku hizi mambo ni tofauti sana, kila mzazi anajua umuhimu wa elimu na kwa kuwa inapatikana kwa urahisi, japo haijakuwa ya kiwango kinachoridhisha, kutokana na serikali kujenga shule nyingi za kata lakini zikiwa haziendi sambamba na kuongeza walimu wa kutosha katika shule hizo, idadi ya watoto wanaoletwa mjini kufanya kazi za ndani imezidi kupungua siku hadi siku.
Hata hivyo, juhudi zetu zilizaa matunda, tulimpata binti ambaye na yeye pia anaye mtoto wa kike makamo ya mwenetu Brian, aliyezalishwa na kutelekezwa huko kijijini kwao Handeni Tanga, alikuja huku mjini kuishi na dada yake binamu lakini inaonekana hakupokelewa vizuri, hivyo ikamlazimu atafute kazi, ambapo aliletwa kwetu.
Alituomba tumpatie nauli ili amrudishe mwanae nyumbani akakae na mama yake ili aweze kufanya kazi kwa ufanisi, tuliafiki, lakini baadae tukaona ni vyema akiishi na sisi pamoja na mwanae kwa kuwa mwenetu alishaanza kuzoeana na hako ka binti ikabidi turidhie abaki na mwanae kama vile kampani kwa mwenetu.
Tulimwambia wazi kuwa pamoja na kumlipa mshahara lakini ataishi na sisi kama ndugu kwa maana akiwa na shida yoyote ile aseme tutamsaidia nje ya mshahara. Alionekana kuwa mpole sana na mwenye nidhamu na wote tulimpenda sana.
Tulikuwa tunampenda yeye na mwanae na tulikuwa tunamuhudumia mwanae sawa na mwenetu, bila ya ubaguzi na tuliamua kumpa pesa akafanye shopping ya nguo zake na mwanae. Lakini kukawa na hali ya uchafu pale nyumbani, na watoto wakawa hawaogeshwi na kama ni kuogeshwa inakuwa ni kuwaloweka tu kwenye maji na hata nguo nazo zikifuliwa hazitakati. Tulijadiliana na mume wangu tukaona labda ni kutokana na kutingwa na kulea watoto, kwani watoto wote walikuwa ni watundu, mwenetu ni mtundu na mwanae pia ni mtundu.
Tuliona ni vyema amrudishe mwanae huko kwao Handeni ili asiwe na majukumu mengi.Tuliandaa nauli na kumweleza kuwa siku mbili zijazo atasafiri kwenda kwao kumpeleka mtoto.
Aliaga kumpeleka mtoto wake akasukwe huko kwa dada yake na tulimruhusu, lakini hapo ndipo tulipokuja kugundua mengi tusiyoyajua.
Hakurudi siku ile na siku iliyofuata tuliamua kufanya usafi wenyewe, dada Yasinta, tulikutana na vitu vya ajabu chini ya kitanda, ambao haufai kuelezea humu. Tulikuta vidonge vya majira pamoja makorokoro mengine ambayo yalikuwa yanatia kinyaa.
Tulishikwa na kinyaa, lakini ni nyumba yetu tutaacha huo uchafu? Ikabidi tusafishe chumba mpaka kikawa kusafi pamoja na kufua nguo zote pale nyumbani ikiwa ni pamoja na za kwake na za mtoto wake.
Tulipozungumza na jirani yetu mmoja ili kujua hali halisi ya pale nyumbani maana sisi wote ni wajasiriamali na hatushindi nyumbani. Kwa kusita sita sana ndio akatueleza. Kumbe kila tukiondoka nyumbani yule binti na yeye anatoka zake kwenda kwa mabwana zake na kurudi mchana lakini anakuwa kambebea mwanae chipsi, na mwenetu Brian anashinda na njaa kwa kuwa hawezi kula chipsi kavu, inatokea watoto wa jirani yetu humpa chakula na kila akiulizwa anasema kuwa eti hatujaacha pesa za matumizi, wakati tulikuwa tunampa pesa za kutosha.
Alikuwa kila siku ananunua nguo mpya na pesa zetu, na kibaya zaidi ilikuwa Brian akilia njaa anamtukama matusi makubwa kama mtu mzima….eti anamwambia ku*****la mama yako msenge wewe sasa unalia nini…….kamlilie mama yako huko…..Hivi hayo matusi anastahili mtoto kama Brian ambaye ndio atatimiza miaka miwili mwezi ujao?
Tulisimuliwa vituko vyake vingi sana mpaka nililia kwa uchungu. Ilipofika usiku ndio akarudi, mume wangu hakuwa na maneno mengi alimlipa mshahara wake wa siku kumi alizoishi na sisi na akamwamuru arudi alipotoka usiku ule ule. Aliacha nguo zake mpaka leo hajaja kuzichukua, lakini kuna siku alikuja mahali ninapofanyia biashara zangu kunisalimia na kuniomba radhi. Alikiri kufanya hayo niliyosimuliwa na aliomba tumpe nafasi nyingine, ila mume wangu amekataa katakata kumpokea tena. Ila nilipomchunguza alionekana kuwa na hali mbaya sana na alinilalamikia kuwa hajala huko kwa dada yake, na hata mtoto wake naye anaonekana afya yake imedorora sana kutokana na kutopata chakula.
Nilishikwa na huruma na nilimpa fedha kidogo ili akamnunulie mtoto chakula.Hivi sasa anatangatanga mtaani na nadhani ashaanza kufanya umalaya kwani kuna siku nilikutana naye majira ya usiku nikitoka kwenye biashara zangu, hizo nguo alizovaa, zinatia aibu, yaani dada Yasinta alikuwa amevaa kinguo kifupii na kiblauzi kilichoacha mgongo na sehemu ya kitovu nje, nilimsimamisha na kumuuliza anakoelekea usiku ule, kwa aibu sana aliniambia kuwa anakwenda kwa rafiki yake.Sikusema kitu nilimuacha aendelee na safari zake na mimi nikajirudia zangu nyumbani kwangu, yaani dada, niliogopa, kumbe nilikuwa naishi na fuska ndani ya nyumba bila kujua. Kusema kweli dada nilibaki na maswali mengi sana ambayo sikuweza kupata majibu yake.
Hivi mtu kama huyo anaweza kusingizia kuwa anafanya umalaya kwa kuwa hana fedha au ni kutafuta fedha kwa njia ya mkato? Je hakuna shughuli yoyote ambayo angeweza kufanya zaidi ya umalaya? Je akipata ukimwi, ni nini hatima ya mwanaye?
Sasa sijui tulifanya ukatili kumfukuza au alistahili
0 Maoni