MAMA ALIPINGA SANA NISIOLEWE, KUMBE



MAMA ALIPINGA SANA NISIOLEWE, KUMBE…..”
Jina langu ni Herieti ninafanya biashara, ningependa nianze masimulizi yangu moja kwa moja kwenye ndoa, kwani bila ndoa nisingefikia hatua ya kusimulia mkasa huu katika maisha.
Niliolewa mwaka 1995, baada ya visa na mikasa mingi sana, ambayo nashindwa kujua hadi leo ni kwa nini sikuweza kuibaini. Visa na mikasa hiyo ilikuwa inatoka kwa mtu ambaye sikutarajia kwamba, angekuwa nyuma ya jambo kama lile-mama yangu mzazi.
Hivi sasa mtu anaponiambia akina mama wengi wa mijini, siku hizi hawana maana, siwezi kabisa kumbishia na niko tayari kukaa naye kutwa nzima tukijadili jambo hilo.
Tangu nilipoanza uchumba na kijana mmoja aliyekuwa akiitwa James, mama alipinga sana nisiolewe naye. Alipinga kwa njia ambayo mtu yeyote angeamini walikuwa na kisa kibaya sana cha muda mrefu.
Nakumbuka baada tu ya kumtambulisha nyumbani, mama alikuwa mchungu sana na jambo hilo, wakati siku zote yeye ndiye alikuwa mstari wa mbele kuniambia nichangamke kuolewa, kauli ambayo ilikuwa ikinikera sana.
Mama aliniambia siku ile ya kwanza kwamba, kuolewa na James labda ni hadi yeye afe. Niliogopa sana aliposema vile na mwanzoni nilidhani ni mzaha. Nilipogundua kwamba hakuwa akifanya mzaha, nilimuuliza sababu ya kumchukia yule kijana, ambaye hawakuwa wakijuana kabla sijamtambulisha. Mama alisema, yule kijana anaonekana kuwa ni mhuni, malaya na hana adabu.
Nilishangaa sana kwani tangu kumfahamu James, sikuona dalili yeyote ya zile tabia alizozisema mama. Alipozidi kusisitiza kwamba, hakubali nikaolewa, nilijua mambo ni magumu kuliko nilivyodhania awali. Nilimwambia kwamba, pamoja na kwamba ni mama yangu, nisingekubali jambo kama lile.
Mama aliendelea kukataa tusioane hadi kufikia mahali pa kufanya kikao na baba yangu. Alipoulizwa sababu, alikuwa akisema tu kwamba, James anaonekana kuwa ni mhuni, hivyo hafai kunioa.
Kutokana na ukweli kwamba, hakuna aliyekuwa akiziona tabia hizo, hakuna aliyemsikiliza mama. Hatimaye tulifunga ndoa na mama alizira mwanzoni kuhudhuria, ingawa dakika za mwishoni alikuja harusini akiwa kama mgonjwa.
Mara baada ya ndoa, ambapo nilihamia kwa James, kule Sinza, ikaanza vita hasa, vita kweli. Mama alianza kuja nyumbani wakati James hayupo. Alikuwa akifika tu ni kuanza kunichamba kwamba sina akili, mimi mhuni na huyo James wangu, na kwamba, nitakoma kwa kujifanya najua kuolewa.
Nilikuwa nanyamaza mara nyingi, bali nikizidiwa na hasira nilikuwa namwomba mama aondoke kwangu. Alikuwa akiniambia, “ukiujua ukweli utarudi kwangu na nitakupokea, mwana asiye na haya.” Nilikuwa najiuliza sana maana ya maneno yale kila wakati.
Siku moja nilimuuliza James kama alikuwa anamfahamu mama kabla sijakutana naye au kuna mtu anamfahamu James vizuri na wanafahamiana na mama. James alisema, ingekuwa anamfahamu mama angeniambia.
“Labda ana wivu. Akina mama wengine wanakuwa na wivu na watoto wao wakiolewa…” Nilimwambia aache kuzungumza upuuzi. “Mama yangu anionee wivu, kwa kutuona kwetu kuna laana au…”
James aliniambia kwamba, siyo wivu kama ninavyofikiria mimi. Alisema ni wivu ambao hutokana na mama kumtamani binti yake aolewe na mtu anayemtaka yeye. James alisema, lakini ndani ya sauti yake kulikuwa na kitu ambacho sikukipenda sana. Kauli hiyo ya pili ilionekana kama ya kujitetea zaidi kuliko kitu kingine. Kauli yake ya kwanza ilikuwa na maana maalumu.
Sikujua ni kitu gani hasa kilinisukuma kuanza kuwa na mashaka kwamba, James alikuwa akimfahamu mama yangu na mama pia alikuwa akimfahamu James. Sikutaka kulitilia nguvu jambo hili, lakini niliona likinisukuma kuamini. Nililidharau na likapotea kwa siku kama nne.
Siku ya tano, mama alifika nyumbani na kuniuliza kama nimeamua, kweli kuharibu maisha yangu kwa kuolewa na mtu ambaye anatembea na watu wazima, bila aibu wala kichefuchefu. Huyu James wakati huo alikuwa na miaka kama 32, mimi nikiwa na miaka 21.
Mama alipekua kwenye mkoba wake na kutoa picha mbili za James akiwa na mwanamke. Lakini picha ya mwanamke ilikuwa imekatwa kichwa. Picha ya kwanza, mwanamke aliyekuwa katika khanga alikuwa amekumbatiana na James. Kwa kuwa kichwa cha mwanamke kilikuwa kimekatwa sikuweza kumtambua.
Picha ya pili ilikuwa ni ya James na mwanamke yuleyule akiwa amevaa kichupi na James akiwa na bukta wakiwa wamekumbatiana tena, bila shaka wakibusiana.
Nilijihisi nikitetemeka. Nilimuuliza mama, “huyo mwanamke mbona maekatwa kichwa?”
Mama alicheka kidogo. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumsikia akicheka tukiwa wawili tangu nilipomleta James nyumbani kumtambulisha. “Nisingekata kichwa, unadhani ungekuwa umekaa kwa amani kama ulivyokaa sasa hivi hapo. Huyu mwanamke hata ukiangalia vizuri hapa unaweza kumjua…” Alisema na kuninyang’anya zile picha.
“Mimi ni mama yako, nikikwambia kwamba, uwe mwangalifu kweli. Huyu mwenzio kazi yake mashangingi yenye pesa hapa mjini. Amezaa na majimwanamke hayana mbele wala nyuma, mradi yana hela...” Mama alisema kwa sauti yenye kuonesha kwamba, hakuwa akitania.
Nilikuwa natetemeka. Nilikuwa nimeamini na nilijiona mjinga. Machozi yalianza kunitoka na mama alinishika na kunibembeleza. “Lengo langu siyo kukuumiza, nataka tu ujue unaishi na mtu wa aina gani ili kabla hujapata ujauzito ujue namna ya kujitetea.”
Sikuwa nasikia kitu, kwani mawazo yangu yalikuwa kwenye zile picha. Polepole nilianza kuhisi jambo. Yule mwanamke kwenye picha zile nilikuwa ninamfahamu. Alikuwa ni rafiki yake mama. Sikumwambia mama kuhusu ugunduzi ule na nilijiambia kwamba, hiyo ilikuwa ni vita yangu mwenyewe, hakuna cha mama wala James.
Nilipopata ahueni, mama aliaga na kuondoka. Nilishindwa kusema lolote. Nilianza kulia na nilijilaumu sana kwa kweli. Niliingia chumbani kujaribu kulala lakini nilishindwa. Nilihangaika hadi James alipokuja kutoka shughulini.
Alipoingia tu nilifungua bomba la machozi. Alishikwa na mshangao na alinifuata kunishika ili ajue kulikoni. Nilimsukuma na sikuweza kusema chochote. “Kuna nini mke wangu, kumetokea jambo gani tena!”Alisema akiwa ameshangaa. Ingekuwa siyo kwa sababu ya kitendo chake kile, ningemwonea sana huruma, lakini.
Nakwambia, sikuweza kuzungumza na James chochote usiku kucha na nililala sebuleni, ambapo naye alikesha nami. Kila nikitaka kusema nilikuwa nahisi kitu fulani kinanikaba kwenye koo. Sikuweza kabisa.
Asubuhi James aliondoka kwenda kwenye shughuli zake. Nilitoka pale sebuleni na kwenda chumbani, Nilijiandaa nikiwa mgonjwa kabisa. Sikuweza kunywa chai, wala sikujipamba kwa chochote zaidi ya kuoga tu.
Niliondoka kwenda mjini saa nne asubuhi. Nilikuwa nimeamua kwenda kwa yule rafiki yake mama, ambaye alikuwa akifanya kazi serikalini (sitataja ofisi). Nilitaka kwenda kumwambia kwamba, nina hasira na kinyongo naye ili anisamehe. Nilijua kwa kumwambia hivyo ningehisi nafuu kubwa.
Nilijua pia labda angenipa moyo kwamba huenda walikuwa tu wako karibu na James na vitu vingine vya aina hiyo. Nilikuwa nataka kupewa moyo, ajabu eh!
Nilifika ofisini na niliambiwa yupo na hakuwa na mtu. Niliwaomba mapokezi nikamwone. Niliruhusiwa kuingia. Nilipoingia alinikaribisha vizuri sana.
Ile kumaliza kumsalimia nilianza kulia. Yule mama alishtuka na kuja kunishika na kuniweka kitini. “Nini tena Herieti, kuna kitu gani, kuna msib…Kuna tatizo gani kubwa, hebu sema. Huna haja ya kulia…” Alinipa moyo na alikuwa anajua kubembeleza. Nilifikiria, kama vile ndivyo alivyombembeleza mume wangu, alikuwa na haki ya kumpata.
“Mama nimekuja, naomba kwanza unisamehe, yaani naomba sana kama nitakuvunjia heshima, unisamehe sana. Mimi ni mdogo, sijui mambo ya ndoa na wanaume, kwa hiyo naomba unisamehe kama nitasema jambo baya.” Nilisema na kupumua.
“Sema tu mwanangu, mbona hujanikosea jambo, sema tu, kuwa huru”
“Mama jana nimefuma picha nyumbani. Ni picha…picha za mume wangu akiwa na mtu kama wewe, yaani huyo mwanamke sehemu ya kichwa imeondolewa, lakini huku chini mnafanana sana….”
Yule mama alishusha pumzi. Badala ya kuwa mkali alisema, “mwanangu, hebu kuwa mkweli nikusaidie. Ni picha umezifuma nyumbani au zimeletwa kwako na mtu, akakuambia huyo mwanamke ni mimi?” Aliuliza kwa utulivu, utadhani jambo lenyewe alikuwa analijua siku nyingi.
Nilimwambia ukweli, kuhusu mama na picha zile. Yule mama alikuwa na busara na hekima kubwa. Aliniambia hivi;
“Hukuniona kwenye harusi yako, lakini hujaniuliza bado. Kama ulikuwa hujui ni kwamba, aikuhudhuria kwenye harusi yako, sababu ni hii. Naomba ujikaze, uukaze moyo wako.” Aliniambia.
Nilihisi nikianza kutoka jasho pamoja na kwamba ofisi ilikuwa na feni. Aliniambia, “hebu vuta pumzi kwa nguvu kwenda ndani na uzitoe nje.” Nilifanya hivyo na kutulia.
“Mama yako alikuwa na uhusiano na James.” Nilihisi kama vile nimeyeyuka na sikuwa mimi tena. “Nilmwambia mama yako akwambie ukweli ili usiingie kwenye maumivu, akakataa kwa sababu bado anampenda James”
“Mimi tulikorofishana pia na kuwa kila mtu kivyake kwa sababu ya huyu kijana. Niliwahi hata kabla hujakutana na James kumwambia kwamba, anajiaibisha bure kuwa na uhusiano na kijana mdogo kama huyu.”
Yule mama alipima maneno yake na kuendelea, “Mumeo hakujua kama yule ni mama yako hadi siku ya utambulisho na akashindwa kusema chochote. Mama yako naye hakujua pia hadi siku ile ulipompeleka nyumbani kumtambulisha. James ndiye aliyemwacha mama yako, wakati mama yako alikuwa bado anampenda…”
Sikuwa nasikia chochote. Nilisimama ili kuondoka, lakini yule mama alinizuia. Alizungumza nami mambo mengi kuhusu ndoa, kuhusu usaliti na kunipa moyo. Ninachomshukuru ni kwamba, aliwatetea James na mama ingawa alisema wana tabia chafu. Nilizungumza na huyu mama kwa karibu saa tatu, hadi tukaenda wote lanchi.
Siku hiyo, sikurudi nyumbani, nilikwenda kwa mjombangu (marehemu kwa sasa), kaka yao mkubwa mama kule Tabata. Nilimfahamisha kila kitu. Kumbe alikuwa na presha, ikapanda. Ilikuwa patashika, lakini alipata nafuu.
Wiki moja baada ya tukio lile, wanandugu upande wa mama walikutana, bila kumshirikisha baba. Alikuwepo James na mama, ambao walilaumiwa na kutukanwa sana na mjomba. Halafu tuliombwa tufanye taratibu za kuachana na James.
Mama tulimzika mwaka 2004. Sijui kama ni kihoro cha jambo hili au vipi, kwani tangu wakati ule alianza kunyong’onyea na kuwa kimya muda mwingi tu. James ameoa na ana watoto wawili, sina uadui naye ila namkwepa kama ukoma na yeye pia ananikwepa, ingawa yeye ni kwa aibu.
Huyu mama jirani yetu, ambaye ndiye aliyenifahamisha kila kitu, yupo na sitaki kusema yuko wapi kwa sababu alikuja kuwa mtu mkubwa. Nikimtaja utamjua tu au utakuwa ushasikia jina lake. Anastahili cheo popote, kwa sababu ana busara.
*****************************

Chapisha Maoni

0 Maoni