una hii dhana ambayo imejengeka kuwa mkifunga ndoa na mtu, mkachuma mali hata kama zina majina ya mmoja wenu basi ni zenu wote.

Kuna hii dhana ambayo imejengeka kuwa mkifunga ndoa na mtu, mkachuma mali hata kama zina majina ya mmoja wenu basi ni zenu wote. Hii mara nyingi inatokea kwa wanawake, unakuta mwanamke anafanya kazi, wananunua kiwanja, anaandika jina la mwanaume na ukimuuliza anakuambia tuna ndoa ya Kanisani/Msikitini/Kiserikali/Kimila. Wengi wanadhani kuwa kwa kufunga ndoa tu moja kwa moja inaifanya ile mali kuwa ya kwao! Jibu ni hapana! Hapana! Hapana!
Kwa mujibu wa sharia ya ndoa ya Mwaka 1971, mwana ndoa anaweza kumiliki mali binafsi. Hapa nifafanue kuwa, mali ambayo ina jina la mume ni ya mume na mali ambayo ina jina la mke ni ya mke na mali ambayo ina majina yao wote basi ni mali ya wanandoa ni ya wote. Sasa ishu ya kugawana ikoje, hapa ndiyo pagumu na hapa ndiyo panawafanya wanawake wengi kutapeliwa. Watu wengi wanaamini kuwa mkiwa kwenye ndoa kila kitu ni chakwenu na mkitaka kuacha basi mtagawana.
Iko hivi, kama kile kitu tuseme nyumba ina majina yenu wote basi mnakua na haki sawa mtagawana nusu kwa nusu bila kujali nani kachangia nini, mali hii mkiahana mtagawana. Lakini mali ambayo ina jina la mmoja wenu bila kujali kuwa nani kachangia nini hii itatambulika kuwa ni ya yule mwenye jina. Kwamba kama nyumba ina jina la mwanaume, hata kama pesa yote katoa mwanamke basi hiyo nyumba kisheria ni ya mwanaume na mkitengana anachukua mwanaume yote.
Najua ushaanza kutoa povu mbona wanagawana? Iko hivi, kama mali ina jina la mmoja wenu, ukitaka kugawana tena si nusu kwa nusu bali kwa kile ulichochangia ni lazima uishawishi mahakama kuwa na wewe ulichangia. Labda useme wakati anajenga mimi nilichukua mkopo ndiyo ukanunua kiwanja, tukajenga, alete ushahidi wake na wewe uweke wako mezani! Sawa, kama huna ushahidi jua ni yake na imekula kwako.
Kama ni Mama wa nyumbani hapa utagaiwa kutokana na mchango wako wa kuwa Mama wa nyumbani na si nusu kwa nusu. Kwa maana hiyo kugawana ni lazima uwe na wakili mzuri ambaye anaweza kuthibitishia mahakama kuwa na wewe ulichangia, zaidi ya hapo unaweza kua wewe ndiyo ulitoa pesa yote ya kujengea lakini jina ni la mwanaume ukajikuta unapata kale kamgao kadogo kakuwa tu Mama wa nyumbani au nako hata usikapate!

Chapisha Maoni

0 Maoni