Moja ya somo kubwa ambalo wanawake wengi hufundishwa kila siku ni uvumilivu. Kila mwalimu wa ndoa ambaye utamsikia tukiianza na Mama anapoongea na binti yake basi humuambia kuwa ndoa ni uvumilivu. Nikweli ndoa ni uvumilivu, lakini kitu kikubwa ambacho watu wengi hushindwa kuwaambia wanawake wengi nikua wanatakiwa kuvumilia nini?
Lakini pia hata wakiwaambia nini cha kuvumilia basi hushindwa kuwaambia ni kwanini wavumilie. Kwa mfano mkulima anapolima anakaa kuvumilia kipindi flani ili apate mavuno, kama ni mahindi basi yaje mahindi na kama ni mtama uje mtama. Anavumilia akijua kuwa ni kwanini anavumilia, anajua kuwa mwisho wa siku atapata kitu flani.
Lakini binti anayepigwa na mume wake anapoambiwa na Mama yake kuhusu kuvumilia kama akimuuliza Mama yake nivumilie nini sanasana ataambiwa hata Baba yako alikua ananipiga kama unavyopigwa lakini kama binti atahoji kidogo na kumuuliza ulipata nini baada ya kuvumilia, sanasana utasikia anasema si unaona mpaka sasa niko naye lakini hatakuambia kuwa mpaka sasa nina furaha!
Lakini kama ukichunguza kidogo utakuta huyo Mama bado anaendelea kupigwa au Baba kaacha lakini ni kwakua kachoka anamtegemea Mama hivyo inabidi awe mpole tu lakini Mama naye hakuna alichopata kwa kuvumilia. Ninachosema hapa nikuwa, watu wengi hufundisha uvumilivu kana kwamba unaweza kutatua matatizo ya Ndoa.
Sana sana ni kuyaahirisha na kuyafungia macho kana kwamba hayapo. Kufumbia amcho au kusema kua tatizo flani halipo kamwe hakuwezi kuliondoa hilo tatizo, linaendelea kuwepo na mmoja kuumia. Ndiyo maana mimi nasema kuwa kama ukiona ndoa yako ina matatizo, badala ya kuvumilia basi hembu angalia namna ya kulitatua hilo tatizo.
Labda mapenzi ya mepungua, mume kaanza kuchelewa kurudi nyumbani, hembu jiulize utafanyaje ili awahi, kama una kitabu changu basi soma sehemu ya tatu. Huna furaha, mume hakujali, umefanya kila kitu kumfurahisha, badala ya kuvumilia basi hembu jifunze namna ya kujitengenezea furaha yako mwenewe na kama una Kitabu changu basi soma shemu ya nne.
Lakini mwanaume anakupiga kila siku, kashakugeuza ngoma, umemshitaki kwa ndugu zake mpaka basi bado anaendelea. Kwanza mpeleke Polisi na kama unaona habadiliki basi ondoka kabla hajakuua. Kuna mambo mengine si sifa kuvumilia, kumsingizia kua eti ana hasira za karibu, hembu muulize kama ana hasira za karibu mbona hata siku moja hazijampanda akampiga makofi Bosi wake au Mama yake ni wewe tu!
0 Maoni