Kataa kuwa mpira wa kona




JUMATANO saafi , Shangingi wenu nimejaa tele kuwaletea ile kitu roho inapenda. Niwape maneno yenu pambe, niwachambe vizabizabina msio na haya wala hamjui vibaya. Kuna tabia za baadhi ya wanawake huwa najiuliza wamezaliwa au wametupwa hapa duniani. Mwanamke kutwa unajipara, unamaliza vipodozi kwa kuwa mpira wa kona haloooo! Unajiona mjanja mwenyewe kubadili wanaume kama vile siti ya daladala, bibi hii ni aibu. Mwanamke uwe na staha kidogo.
Uwe na haiba ya kike, sio wewe macho makavu unawamaliza tu wanaume mpaka wengine wanakuja kujuana, mnatudharaulisha. Tunaonekana wote mwalimu wetu kipofu sababu ya ujinga wenu. Hivi unajisikiaje unapokutana na wanaume zaidi ya kumi na wote umeshalala nao? Jamani ashakum sio matusi lakini tunatia kinyaa.
Mwanamke unakuwa kama jamvi la wageni yaani kama maharage ya Mbeya, huwezi kusema hapana kila kitu hewala. Mwanaume hata akikutania tu wewe unamkumbushia afanye kweli mh, sijui mkoje jamaniii! Mwanamke inafi ka mahali hata marafi ki zako wanaogopa kukutambulisha kwa wapenzi wao maana wewe macho juu utadhani dereva wa trekta. Badilika bibi maisha sio kuwa na msururu wa wanaume, maisha kuwa na fedha. Mwanamke kuwa na heshima ya biashara basi.
Uwe bize sio kutwa kushinda vibarazani, wewe unajiaibisha mwenyewe. Wenzako wamejituliza wanaolewa, wewe kutwa kutanga na njia; Kariakoo, Manzese, Buguruni wanakujua wewe inakusaidia nini? Umaarufu maandazi nani anautaka? Umaarufu uwe wa hela, umaarufu uwe wa kuajiri watu wakufanyie kazi. Umaarufu wa kunuka kwapa nani anautaka. Mwanamke anajishughulisha, mwanamke anajua mipango ya mjini sio mipango ya kusutana. Mwanamke unawaza vigodoro kila siku inahusu?
Nakupasha bibi upashike tena kwa maji ya moto. Nyinyi ndio kutwa kuchukua waume za watu na kuishia kuzalishwa na kutelekezwa. Eeeh, mnatelekezwa halafu kutwa kuanza kulialia, umeyataka mwenyewe, ulitumwa kuzaa bila mpangilio? Unazaa na mume wa mtu na unajua ana familia yake aliyosota nayo tangu
akiwa hana kitu unadhani atakujali wewe mliyekutana tu kwa muda mfupi? Atakuacha mchana kweupe bibi, hata kama ni njaa sema nayo kidogo. Jipe nafasi japo ya kutafakari maisha yako bibi. Ujue umetoka wapi na unakwenda wapi. Sio wewe mwaka jana kama mwaka juzi na mwaka ujao kama mwaka jana tu upo hapo? Raha ya maisha mwanamke uwe na mwanaume wako sio kubadilibadili kama spea za gari.
Utachezewa wewe na wanaume halafu mwisho wa siku utabaki kama watembea mtupu barabarani. Watu kila mahali wanazo habari zako, wanakuanika tu jinsi ulivyo. Jipange uwe mwanamke mwenye heshima zake bibi, 2020 ndiyo hiyooo usimlaumu mtu kama maisha utayakosea mwenyewe. Sema na njaa yako bibi, Anko Magu bado tunaye ndio rais na bado yupo yupo sana tu. Tafuta hela acha kuwategemea wanaume. Jamani kwa leo Shangingi naweka nukta, inshaallah tukutane wiki ijayo hapahapa niwape kitu roho inapenda. Jamani nawapenda!

Chapisha Maoni

0 Maoni