Mapenzi ya dhati ni uaminifu kati ya wapendanao

Ukatili unavyoweza kuondoa uaminifu na kuharibu mapenzi kati ya wapendanao


Mapenzi ya dhati ni uaminifu kati ya wapendanao


Hasan alikuwa kijana mdogo aliyeachwa yatima baada ya baba yake kufariki jeshini.
Mamake Hasan aliyejulikana kwa jina la "Karaca" alimkabidhi mwanawe kwa mwanakijiji mmoja aliyeitwa Serdengeçti Osman Ağa ili amlee kama babake mlezi. Hasan alipofikisha umri mkubwa, alitaka kuozeshwa binti mmoja asiyekuwa na familia kijijini.
Hasan aliyetambulika kwa jina la Karacoğlan hakutaka kuoa ingawa hakumwambia babake mlezi Osman Ağa.
Aliwaza na kuwazua kuhusu uamuzi huo hadi siku ya harusi kuwadia lakini hakupata ufumbuzi.
Licha ya maandilizi ya harusi kukamilika, Hasan akaamua kutoroka kijijini.
Hasan Karacaoğlan aliyetorokea milimani hakujulikana sehemu aliyokwenda wala mipango yake ya baadaye aliyokuwa nayo.
Badala ya kufungasha mizigo ya nyumbani, Hasan alibeba ala yake ya muziki (Saz) pekee.
Baada ya kuchoka kutokana na matembezi ya muda mrefu, akadondoka chini ya mti mmoja uliokuwa na kivuli na kutekwa na usingizi.
Usingizi akaota ndoto ambapo alimuona babu mmoja akimpa bakuli na kumwambia hivi: ‘Kunywa ili ukate kiu na kuondoa machofu.
Kinywa chako kiwe kama chiriku na moyo wako upate faraja.’ Baada ya Karacoğlan kunywa kile kilichokuwa ndani ya bakuli lile, akahisi mwili wake umepata nguvu upya.
Ghafla akaamka na kuichukuwa ala ya yake ya muziki aliyokuwa amelalia kama mto na kuanza kupiga. Akaanza kuhisi msisimko moyoni mwake uliozidi kumfanya kutaka kuendelea kucheza ala yake ya mziki.
Aliendelea kuimba hata alipofika katika eneo la Türmen lililoko milimani.
Wakazi wa Türmen walimpokea na kumkaribisha Karacaoğlan kwa furaha. Karacaoğlan alivutia wengi kwa sauti yake nzuri aliyoimbia wimbo wa mapenzi.
Kila alipoanza kucheza ala yake ya muziki na kuimba, yeyote aliyesikia sauti yake alitulia tuli na kusikiza. Hata wachungaji mifugo walioko milimani pia waliacha shughuli zao na kuja kumsikiza Karacaoğlan.
Inadaiwa kwamba sauti yake ilikuwa ni kama yenye miujiza ambayo haikusikizwa na binadamu pekee bali na viumbe vyote kama vile miti, wadudu, ndege na wanyama.
Baada ya muda mrefu, Mwenyezi Mungu akamkutanisha Karacaoğlan na binti mmoja mrembo aliyeitwa Elif.
Wapenzi hao wawili walipenana kwa dhati ingawa babake ElifBoran Bey hakupendelea wawili hao kuwa pamoja. Kutokana na hali hiyo, Karacaoğlan akasubiria wakati ambapo Elif na babake hawapo nyumbani na kutoroka kisirisiri.
Karacaoğlan akafunga safari nyingine tena na kufikia mji wa Karaman. Wakati huo huo, Boran Bey ambaye hakupenda kumuona binti yake Elif akihuzunika, akaamua kumfuata Karacaoğlan na kumrudisha ili awe pamoja na Elif.
Hatua hiyo ilimstaajabisha sana Karacaoğlan na kumletea furaha isiyo kifani. Lakini baada ya muda mfupi, wapenzi hao wakaamua kutoroka usiku mmoja na kwenda katika mji mmoja wa mbali waliopokewa na Tuğrul Bey.

Walipokewa vizuri na Tuğrul Bey katika mji huo na kupewa hifadhi. Kisha Tuğrul Bey akawafanyia harusi wapenzi hao wakafunga pingu za maisha.
Karacoğlan alikuwa akishughulika na sanaa ya muziki huku Elif akifanya kazi za nyumbani. Hivyo ndivyo walivyojikimu kimaisha.
Kama tunavyofahamu maisha hayakosi mitihani na misukosuko, hivyo ndivyo yalivyokuwa maisha ya Karacaoğlan na Elif. Katika mji ule walikoishi, kulikuwa na mtu mmoja kwa jina la Köse aliyempenda Elif.
Baada ya kuwaandama wapenzi wale kwa muda mrefu, mtu huyo alizidiwa na wivu na usiku mmoja akaamua kumvamia Elif wakati Karacaoğlan alipokuwa hayuko nyumbani.
Elif hakutarajia tukio hilo, akaanza kuwaza kwa kuhofia aibu anayoweza kuipata iwapo angetoa ukemi kwa ajili ya msaada wa majirani.
Hakutaka kuabika na pia alihofia kwamba majirani wanaweza kumfikiria vibaya na hata Karacaoğlan kumkasirikia.
Hivyo basi, Elif akaamua kujisalimisha kwa mtu yule na kukaa kimya bila ya mtu yoyote kugundua kilichomtokea.
Wakati huo huo, Karacaoğlan aliyekuwa akicheza ala yake ya muziki kwenye sherehe ya harusi aliyoalikwa, akakumbwa nam kasa! Kwa bahati mbaya nyuzi ya ala yake ya muziki ikakatika ghafla.
Kutoka na kutokuwa na nyuzi ya ziada, Karacaoğlan akanyanyuka na kukimbia nyumbani ili afuate nyuzi nyingine. Karacaoğlan akapigwa na butwaa kumkuta Elif na mtu yule kitandani wamelala pasi na kujitambua.
Kinywa chake kiliganda na kupoteza nguvu zote asijuwe la kusema. Akaamua kuchukuwa shuka na kuwafunika kisha akaondoka.
Baada ya Elif kuamka na kuona kuwa wamefunikwa shuka, akajuwa kwamba Karacaoğlan alikuja nyumbani na kuwaona.
Alitambua kwamba Karacaoğlan ametokomea zake na wala hatorudi tena.
Elif sasa alikuwa hana tena la kusema na mwishowe akashindwa kuficha siri na kumsimulia mamake mkasa huo. Mamake Elif aliposikia mkasa huo uliomkumba binti yake, akamuua mtu yule aliyesababisha kuvunjika kwa ndoa ya Karacaoğlan na Elif.
Baada ya kiongozi wa mji kupata habari za mauaji na mkasa mzima uliosababisha, alihuzunika na kumuhurumia Karacaoğlan kisha akatuma watu kwenda lkumtafuta kote mjini. Miaka mingi ilipita lakini Karacaoğlan hakuonekana.
Hata hivyo Karacaoğlan alikuwa tayari anazo habari za kutafutwa na mkuu wa mji kutokana na mkasa uliomkuta. Siku moja akaonekana mjini Antep akicheza ala ya muziki.
Baadhi ya watu wanasema kwamba Karacaoğlan alionekana Akkoyunlular ilhali wengine wanadai kuwa katika jangwa la Yemen, wengine nao wanasema alikuwa Karadeniz. Kila watu walipofika katika sehemu walizosikia fununu za kuwepo kwa Karacaoğlan, hawakuweza kumuona ispokuwa kusikia nyimbo zake alizowaachia.
Elif na mkuu wa mji walikuwa wameapa kung’ang’ana hadi kumpata Karacaoğlan aliyepotea katika ulimwengu huu.
Baada ya muda, mkuu wa mji akafariki na kumwacha Elif asijue la kufanya.
Elif hakupoteza matumaini kwa kuwa aliamini kwamba ipo siku Karacoğlan atajua ukweli wa mambo na kurudi nyumbani.
Amini usiamini, dua ya Elif ikakubaliwa! Karacaoğlan alijua ukweli wa mambo na punde alipoamua kurudi mjini kumfuata Elif baada ya miaka mingi, hakuweza kumpata.
Badala yake, Karacaoğlan alionyeshwa kaburi la mpenzi wake wa dhati Elif.
Alihuzunika na kukaa juu ya kaburi la Elif huku akitokwa na machozi. Alitoa ala yake ya muziki na kuimba wimbo huu;
"Tangu kuja kwangu katika dunia hii ya uongo,
Na kunywea bakuli wakati nilipokuwa hai.
Mwanamke amebainisha hatima yangu,
Akanifanya gofu wakati wa kufunga nyuzi yangu..''
Kisha Karacaoğlan akakata nyuzi ya ala yake ya muziki na kujinyonga nayo.
Wakazi wakaamua kumzika karibu na kaburi la Elif kutokana na mapenzi yao ya dhati.
Wakazi wa eneo hilo wanasema kwamba kila mwaka katika msimu wa kipupwe, nuru mbili, moja ya rangi ya kijani na nyingine ya rangi ya samawati hupaa na kuungana angani.
Nuru hizo ni nuru za mapenzi ya Karacaoğlan na Elif.

Chapisha Maoni

0 Maoni